Kitendo cha mashabiki wa yanga kuwafanyia vurugu baadhi ya mashabiki wa simba chausikitisha uongozi wa klabu hiyo.

 UONGOZI wa klabu ya Yanga umesikitishwa na kitendo kisicho cha kiungwana kilichofanywa na baadhi ya mashabiki wao cha kuwapiga na kuwafanyia vurugu baadhi ya mashabiki wa Simba waliofika kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro jana Septemba 27, 2020 kushuhudia mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar.

Pamoja na kusikitishwa, pia uongozi wa Yanga umelaani vikali tabia hiyo inayojengeka ya uvunjifu wa amani katika soka na kuviomba vyombo vya Ulinzi na Usalama kuchunguza na kuwachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.

“Yanga tunaamini Mpira ni furaha na sio uadui na tunawakumbusha mashabiki wetu kwamba upinzani wetu na Simba unatokana na Utani wa Jadi na siyo uhasimu” alisema Wakili, Simon Patrick Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga.

Aidha, uongozi wa Yanga umewashukuru Wanachama na Mashabiki wa Morogoro kwa kujitokeza kwa wingi kushudia mchezo huo, uliomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa goli 1-0, goli lililofugwa na Lamine Moro dakika ya 61′