Na Rhoda Simba,Dodoma.
KATIBU Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Christopher Kadio ameutaka uongozi wa chama cha TPS SACCOS kuwa wabunifu Katika uendeshaji sanjari na kuhamasisha wengine kujiunga na chama hicho ili kuwawezesha kufikia malengo ya pamoja.
Kadio ametoa wito huo leo November 18,2021 jijini hapa wakati alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa Tisa wa Magereza SACCOS uliofanyika makao Makuu ya Jeshi hilo.
Amesema viongozi hao wanapaswa kuwa wabunifu wa namna ya kuendeleza SACCOS yao kwa kuzingatia dhana ya uzalishaji mali ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya ushirika jambo ambalo litasaidia kuwa na maendeleo.
“Niwapongeze sana kwa hatua hiyo na ili chama chenu kiweze kuendeshwa kwa tija lazima kuzingatia sheria namba sita ya vyama vya ushirika ya mwaka 2015 hivyo simamieni hii saccos vizuri “
“Pia uongozi wa chama niwasihi kwamba ili chama kiweze kufanya vizuri lazima kipewe kipaumbele huku mkipaswa kuendana na kasi iliyopo hasa kutoa elimu ya ushirika,kushirikisha wanachama juu ya bajeti ya chama.”alisema Kadio.
Ramadhan Mbezi afisa mikopo wa chama cha TPS SACCOS amesema kumekuwa na mafanikio mengi ambayo wanachama wanapaswa kujivunia chama chao kupata mikopo kwa wakati ambapo mpaka kufikia oktoba mwaka huu tayari wanachama elfu 2,258 wamekopeshwa kiasi cha shilingi bilioni 3.3 Katika mkopo wa dharura.
Pia amesema tayari kiasi cha bilion 8 kimetolewa kwa wanachama 872 kama mkopo wa maendeleo jambo ambalo litawasaidia kutatua shida zao kwa wakati.
Akielezea changamoto amesema hapo awali ilikuwa ni urejeshaji wa mkopo wa dharura lakini kupitia elimu ambayo wamekuwa wakiitoa na mfumo wa kupitia kwa mwajiri wao imesaidia kuondoa changamoto hiyo.
“Tuna mikakati mikubwa ni kuhakikisha wanachama wote wanajiunga ambao ni askari wastaafu na wenza wetu na kwa Sasa tuko elfu 11000 huku Jeshi lina askari 12000 hivyo tunataka kuwafikia wote ili waweze kunufaika na SACCOS hii ambayo ina riba nafuu na kupata mkopo mkubwa ili waweze kutimiza malengo yao “amesema Mbezi.
Kwa upande wake mwanachama Hassan Rashid amesema kuwa Chama hicho kimewasaidia hasa Kwa upande wa faida kwani SACCOS imeleta fursa kwao ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za mikopo mbalimbali ambapo Wengi wamewezeshwa kujenga nyumba za kisasa na mambo mengine ya maendeleo.
Amewataka watu kuchangamkia fursa ya kujiunga kwenye chama hicho ambacho kitakuwa kichocheo katika kutatua shida zao kuliko kwenda kukopa nje ambapo Kuna riba kubwa.