Mahakama kuamua leo kuhusu hatima ya mrithi wa ubunge jimbo la tundu lissu

Hatima
ya kuapishwa kwa mbunge mteule wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji
Mtaturu (CCM), itajulikana leo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam kuamua iwapo itatoa zuio la kuapishwa kwa mbunge huyo ama la.




Katika
maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na kaka wa aliyekuwa mbunge wa
jimbo hilo, Tundu Lissu, Alute Mungwai Lissu, pamoja na mambo mengine,
ameiomba Mahakama hiyo itoe zuio la kuapishwa kwa mbunge huyo mpya na
ruhusa ya kumshtaki Spika wa Bunge, Job Ndugai, kwa kumvua ubunge pasipo
sababu za msingi.




Awali
Mahakama hiyo ilitupilia mbali mapingamizi yaliyowekwa na upande wa
Jamhuri uliotaka kesi hiyo isisikilizwe mahakamani hapo, kutokana na
walichodai ni mapungufu ya kisheria ya maombi hayo, hivyo kutaka
yasisikilizwe.




Jaji
wa Mahakama Kuu, Sirilius Matupa, aliyatupa mapingamizi hayo baada ya
kusikiliza hoja za pande zote mbili kwa maelezo kwamba upande wa Jamhuri
haukuwa na hoja za msingi za kuizuia kesi hiyo isisikilizwe mahakamani
hapo, hivyo kukubaliana na hoja za Wakili wa Lissu, Peter Kibatala.