Makonda awataka watendaji arusha kukaa mguu sawa

Naibu Katibu Mkuu CCM bara John Mongela (kushoto) akimkabidhi Ofisi  Mkuu wa Mkoa Arusha Paul Makonda

Ripoti ya Egidia Vedasto,

Arusha.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha,p Paul Makonda amewataka watendaji kuendana na kasi yake ili kuharakisha maendeleo na kufanikisha malengo ya ilani ya chama.

Akizungumza katika makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika hapa jijini Arusha amesema kwamba watendaji wengi wamekuwa wakifanya kazi chini ya kiwango hali inayochangia migogoro ya wananchi na malalamiko yasiyo kikomo.

Rc Paul Makonda akiwasili Arusha 

Aidha ameeleza kwamba  kuanzia leo ameanza utendaji hivyo watendaji wote wakae mkao wa utayari na kuwajibika sawasawa kila mmoja kwa nafasi yake.

“Mimi ni kiongozi wa wanyonge nina hofu ya Mungu na sipendi kuona wananchi wanalalamika, sitakuwa tayari kushuhudia machozi ya watu kwa sababu ya uzembe” ameeleza Makonda.

Ameendelea kuwakumbusha wakuu wa wilaya, makamishna na wakurugenzi wa idara mbalimbali kufanya kazi kwa makini na kwa wakati ili kumaliza changamoto zinazoukabili mkoa wa Arusha.

Hata hivyo amekumbusha Kamishna wa ardhi kumaliza migogoro yote kwa miezi mitatu sambamba na hayo amemtaka Kamishna wa uhamiaji wa mkoa kutoa pasi za kusafiria (Passport )ndani ya siku saba badala ya siku 14 au zaidi kama ilivyo sasa.

“Watumishi niwakumbushe kwamba nafasi zenu ni dhamana, ukitenda kinyume na haki  ni laana na hata vizazi vyenu baadae vinakuwa vya ajabu kumbe ulitumia vibaya nafasi yako kwa kutoa watu machozi” ameongeza Makonda.

Pia ameeleza mpango mkakati wa kufanya mji kuwa mzuri, kwa kuweka taa za barabarani, kufunga kamera, na kuhakikisha watu wanaojiita wadudu au tatu mzuka wanakuwa watu wema watakaogeuka wachapakazi ili wananchi wote pamoja na watalii wanafika Jijini  kuwe na usalama kwani hawaji huku kulala bali wanakuja kufurahia muda wote.

Hata hivyo amewakumbusha shirika la nyumba la Taifa (NHC) na wananchi wengine kuhakikisha wanaboresha muonekano wa majengo ikiwemo kupaka rangi na kubomoa majengo yaliyochoka ili kuweka mpango wa ujenzi wa Maghorofa, ikiwa ni moja  ya njia ya kuupamba mji.

Awali akimkabidhi Ofisi hiyo, aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Arusha na baadaye kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu CCM Bara  John Mongela amemuahidi Makonda kumpa ushirikiano katika utendaji kazi wake.

Mongela amewataka watendaji kuwa waadilifu na kuonyesha ushirikiano kama walivyofanya kwake.

“Ukweli ni kwamba watendaji wa hapa Arusha wako vizuri katika  kushirikiana lakini wasisahau mimi sio kama wewe, mimi nina kujishaurishauri lakini wewe unachukua hatua haraka mno, watendaji kuweni makini” amesisitiza Mongela.

_Mamia ya wakazi wa mkoa wa arusha wakiwa katika viwanja vya ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha wakimsikiliza Makonda