Marekani yajiandaa na shambulizi la kulipiza kisasi kutoka iran… wanajeshi wengine 3500 kutumwa mashariki ya kati

Marekani
kwa sasa inajiandaa na shambulizi la kulipiza kisasi kutoka Iran baada
ya shambulizi lake la anga kumuua kamanda mkuu wa Iran, hatua ambayo
imetia wasiwasi nchi zote duniani na hata kutiliwa shaka na baadhi ya
wabunge wa Marekani.

Shambulizi la anga la Marekani Alhamis lilimuua Meja Jenerali Qassem
Soleiman, mkuu wa kikosi cha Quds, pamoja na kamanda wa wanamgambo wa
Iraq, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad, na kuchochea
vitisho vikali vya kulipiza kisasi kutoka kwa Kiongozi Mkuu wa Iran
Ayatollah Ali Khamenei.
Ikijibu tishio hilo linalozidi kuongezeka dhidi ya wafanyakazi na vituo
vya Marekani katika Mashariki ya Kati, wizara ya ulinzi ya Marekani
imetoa taarifa ikisema itasambaza kikosi huko Kuwait kama hatua ya
tahadhari na sahihi, bila kutaja idadi ya wanajeshi. 


Hata
hivyo vyombo vya habari vya Marekani jana vilitangaza kuwa nchi hiyo
itatuma zaidi ya askari 3,500 wikiendi hii. Na askari wengine wa ziada
kutoka divisheni ya 82 ya askari wa parashuti watapelekwa Iraq, Kuwait
na sehemu nyingine za kanda hiyo.