Marekani yapinga icc kuichunguza israel

Waziri wa Mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo amesema nchi yake inapinga vikali uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Uhalifu Kivita ICC wa kufungua uchunguzi dhidi ya uhalifu unaotuhumiwa kufanywa na Israel.


Pompeo amesema hatua hiyo iliyotangazwa jana na mwendesha mashtaka mkuu wa ICC inatafuta njia za kuielenga Israel katika namna isiyo ya haki.

Uamuzi huo wa ICC wa kufungua uchunguzi kamili wa madai ya uhalifu wa kivita katika eneo la mamlaka ya ndani ya Palestina umezusha majibu ya hasira kutoka Israel, mshirika mkuu wa Washington kwenye kanda hiyo.

Wapalestina wameukaribisha uamuzi huo waliosema umechelewa kufuatia uchunguzi wa awali wa karibu miaka mitano tangu kuzuka kwa mapigano katika Ukanda wa Gaza mwaka 2014.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameutaja uamuzi wa mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague ambayo Israeli imekataa kujiunga nayo tangu ilipooundwa mwaka 2002, kuwa “Silaha ya kisiasa” dhidi ya taifa hilo la kiyahudi.

Netanyahu pia amesema mahakama ya ICC haina uwezo wa kuchunguza yanayotokea ndani ya mipaka ya Palestina.

“Nimeridhika kuwa ipo sababu ya msingi ya kuendelea na uchunguzi kuhusu hali ndani ya Palestina” alisema mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou Bensuda na kuongeza kuwa amejiridhisha kuwa uhalifu wa kivita umefanywa au unaendelea kufanywa ndani ya Palestina.

Bensouda amesema kabla ya kufungua uchunguzi kamili, ataitaka mahakama ya ICC itoe uamuzi kuhusu uwezo na mipaka yake katika mamlaka ya ndani ya Plaestina kwa sababu eneo hilo lina mizozano mikubwa ya kisheria na uhalali wa udhibiti wa maeneo.

Amesema tayari  ameomba uthibitihso wa eneo analotaka kufungua uchunguzi linalojumisha Ukingo wa magharibi ikiwemo Jerusalem Mashariki na ukanda wa Gaza.

Bensouda amesisitiza lakini kuwa hategemei ruhusa ya majaji wa mahakama hiyo kufungua uchunguzi kwa sababu kumekuwa na maombi kutoka kwa wapalestina wenyewe ambao walijiunga na mahakma hiyo mwaka 2015.

Kwa upande wake Marekani kupitia Pompeo imesema haiamini kuwa Palestina kuwa taifa huru na hivyo haina sifa ya kuwa mwanachama kamili wa mashirika na taasisi za kimataifa ikiwemo mahakama ya ICC.

Suala la uchunguzi dhidi ya Israeli ni mwiba mchungu. Mshauri wa zamani wa taifa wa masuala ya ulinzi John Bolton alitishia mwaka uliopita kuwakamata majaji wa mahakama ya ICC iwapo watafungua uchunguzi dhidi ya Israel au Marekani.

Israeli na Marekani zote zimekataa kujiunga na ICC iliyoanzishwa kama mahakama ya kimataifa ya kushughulia makosa makubwa ya uhalifu ulimwenguni ikiwemo ya kivita na yale dhidi ya ubinadamu.~

Credit: DW