Mbunge wa Ngorongoro Emmanuel Ole Shangai |
Ujumbe wa Mbunge wa Ngorongoro Emmanuelle Ole Shangai
Maisha yangu na familia yangu yapo matatani.
Jana usiku askari walivamia bomani kwangu Endulen na kuwasumbua familia yangu, huku wakitamka maneno kadhaa ya kuonyesha kutishia uhai wangu, mkuu wa msafara aliyekuwa na t-shirt nyekundu ambaye ndiye mkuu wa msafara, akisema mkimkuta huyo mbunge mpigieni Risasi ya mguu au popote tumalizane .
Baada ya tukio hilo Jana, nilimpigia Bw.Kakwaya ambaye ni afisa upelelezi wilaya ya Ngorongoro, na kumtaka kuwa kama wananihitaji Mimi waache usumbufu kwa familia yangu Mimi nitaenda kesho kwa ajili ya mahojiano, lakini kilichonishangaza ni kwamba anasema mahojiano yatafanyika karatu badala ya makao makuu ya Wilaya ya Ngorongoro lakini hiyo haikunipa shida kwa sababu kote ni Tanzania.
Lakini, muda huu wa saa Kumi na dakika Kumi na tatu, Askari wakiwa kwenye magari matatu wamefika Tena nyumbani kwangu huku wakiwa na askari wa kike kwa lengo la kutaka kumkamata mke wangu, huku yeye akiwa hana hatia yeyote .
Napenda kuwajulisha Wanangorongoro wenzangu na Watanzania kwa ujumla kuwa Maisha yangu yapo matatani na usalama siyo salama kabisa .
Rai kwa jeshi la polisi kama mnanitaka Mimi hakuna haja ya kumsumbua mke wangu au mwanafamilia yeyote .
Nilishamwambia afisa upelelezi wilaya ya Ngorongoro kuwa nitakuja kesho kwa ajili ya mahojiano, lakini kwa Hali ilivyo Sasa ni kutishia Maisha yangu. Tatizo hili linatokana na shutuma zilizoandikwa na gazeti la Jamvi la habari kuhusiana na vurugu zilizotokea kwenye mnada wa Endulen, habari ambazo kupitia waandishi wa habari nilishatolea maelezo yangu na kama jeshi la polisi wangetakiwa kutumia njia za kisheria kunitaka kwenda kutoa maelezo yangu na siyo kuja nyumbani kwangu ni mitutu ya bunduki, Jana usiku mama yangu mzazi alizimia na mpaka Leo hajurudi kwenye Hali yake ya kawaida,
Naomba Wanangorongoro wenzangu na Watanzania wenzangu mtambue kuwa sijahusika kwa namna yeyote kwenye vurugu zilizotokea kwenye mnada wa Endulen.
Naomba kuwasilisha kwenu, kama Kuna lolote litanitokea mjue kuwa ni maelekezo ya DC wa Ngorongoro na mkuu wa mkoa wa Arusha.
Emmanuel Lekishon Shangai
Mbunge Jimbo la Ngorongoro.