Meya wa manispaa ya songea awataka wafanyabiashara wa maduka kufungua maduka yao.

   NA AMON MTEGA_ SONGEA.

KUFUATIA Mgomo uliyofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wa maduka na usafirishaji wa abiria katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma Meya wa Manispaa hiyo Michael Mbano amewataka wafanyabiashara hao kufungua biashara zao (Maduka)ili Wananchi waendelee kupatiwa huduma.

Mbano akizungumza ofisini kwake amesema kuwa anashangaa kuona baadhi ya wafanyabiashara kufanya mgomo usiyokuwa na maelezo kamili kwa kuwa hata ofisini kwake hakupatiwa taarifa hizo za uwepo wa mgomo huo.

 Amesema kuwa kama ni madai ya masuala ya kituo cha mabasi (Stendi )iliyopo kata ya Shuleyatanga haina mahusiano na wafanyabiashara wa maduka inashangaza kuona nao wapo kwenye mgomo huo hasa wale wenye maduka ya katikati ya mji.

 Amefafanua kuwa kwa wafanyabiashara wa maduka waliyopangishwa kwenye vibanda vya Manispaa kama wataendelea kutokuzifungua biashara zao basi hatua za kisheria zitafuata ikiwemo pamoja na kuwaondoa kwenye vibanda hivyo.

 “Siwatanii hata kidogo Manispaa imejipanga kuhakikisha huduma zinatolewa kwa wananchi hivyo pasiwepo baadhi ya wafanyabiashara kujiingiza kwenye mambo ambayo hayastahili”Amesema Mbano.

 Akizungumzia suala la baadhi ya wafanyabiashara wa usafirishaji abiria hasa wadaladala mpango uliyokuwa umepangwa na manispaa licha ya kutanua mji ilikuwa ni pamoja na kuwalinda watu wa daladala ,bodaboda na bajaji kwa kuwa nao wanajiingiza kwenye migomo bila kujua wanagomea nini wataona namna nyingine ambayo itakayo faa.

 Hata hivyo kufuatia mgomo huo Serikali ngazi ya  Wilaya ya Songea kupitia kaimu mkuu wa Wilaya hiyo Cosmas Nshenye imetoa masaa 24 kwa wafanyabiashara hao waweze kufungua biashara zao hadi sasa baadhi yao wameshafungua biashara zao hasa maduka yaliyopo pembezoni mwa mji.

Nshenye wakati akitoa maagizo hayo amesema kuwa  licha ya kutoa masaa 24 ya kutaka biashara hizo zifunguliwe  lakini bado amesitisha vibali vya wasafirishaji wa magari ya abiria ya kutoka Songea mjini hadi Mbinga mjini na amewaigiza mamlaka ya usafirishaji abiria Nchi kavu (LATRA)kupokea maombi upya kwa wafanyabiashara watakao hitaji kufanya ruti hiyo.