Na Mwandishi Wetu, Nairobi
MKIMBIAJI maarufu wa mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Conseslus Kipruto yuko hatiani kufungwa miaka 20 baada ya kushtakiwa katika mahakama ya Kapsabet kwa kujihusisha kimapenzi na msichana aliye na umri wa miaka 15.
Kipruto, ambaye atagonga umri wa miaka 26 itakapofika Desemba 8, ameshindia Kenya medali za dhahabu katika mashindano ya Olimpiki, Jumuiya ya Madola na Bara Afrika.
Alifikishwa mahakamani Jumatatu, wiki tatu baada ya ripoti za kudaiwa kufanya mapenzi na msichana huyo mdogo ambaye majna yake yanahifadhiwa.
Alikuwa amepata Uhuru kwa muda wakati wazee na baadhi ya maafisa wa riadha kutoka Bonde la Ufa pamoja na wanariadha kadhaa walipoingilia kati kuzungumza na familia ya msichana huyo wa kidato cha pili katika kaunti yao ya Nandi kutatua kesi hiyo nje ya mahakama.
Mamia ya watu waliokuwa na hasira waliandamana nje ya mahakama ya Kapsabet wakiwa wamebeba mabango wakitaka Kipruto achukuliwe hatua kali ya kisheria.
Umati huo wa watu ulifika mapema nje ya mahakama hiyo ukikashifu nyota huyo kwa kutumia mamilioni ya shilingi anayopata katika utimkaji wa mbio kama chambo kuharibia maisha wasichana ambao hawajafikisha umri wa mtu mzima ambao bado pia wanasoma.
Wanahabari na umma ulisubiri kwa muda mrefu kabla ya Kipruto kuwasili akitumia gari ambalo mtu hawezi kuonekana akiwa ndani. Aliingizwa katika gari la aina ya Pajero ambalo lilimsafirisha hadi katika majengo ya mahakama hayo.
Alikuwa ameficha uso wake kwa kuvalia miwani na barakoa na jaketi iliyokuwa na kofia.
Conseslus alikabiliwa na mashtaka mawili alipofika mbele ya hakimu DA Ocharo. Hakimu alieleza alikuwa akihisi vibaya na alihitaji kuenda hospitalini na akaahirishwa kesi hadi Mei 10, 2021, lakini baada ya kuachilia Conseslus kwa dhamana ya Sh200,000 na mdhamini wa kiasi sawa na hicho.
Mkimbiaji huyo aliwakilishwa na wakili Joshua Lagat. Kesi hiyo inasema kuwa kati ya Oktoba 20 na Oktoba 21 katika kijiji cha Tironoi eneo la Mutwot katika kaunti ya Nandi, Kipruto alifanya ngono na msichana huyo. Kosa la pili ni kuwa kitendo hicho kilikuwa kinyume na maadili.
Kamishna wa Kaunti ya Nandi, Geoffrey Omoding alikuwa ameamrisha Conseslus akamatwe baada ya watu kulalamika kuwa mwanariadha huyo amedhulumu kimapenzi wasichana kadhaa na alikuwa akitumia fedha zake kuhujumu utafutaji wa haki.
Omoding alikashifu maafisa wa polisi waliochukua wiki tatu kutia nguvuni Conseslus, ambaye alisemekana alikuwa ameenda mafichoni tangu achafue wasichana wawili.