Mkoa wa shinyanga kinara mauaji ya wanandoa 2021

 Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mkoa wa Shinyanga umetajwa kuwa na ongezeko la vifo vya wanandoa  vitokanavyo na wivu wa mapenzi ambapo takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi cha Januari – Oktoba mwaka huu 2021 kuna idadi ya watu 12 waliopoteza maisha kutokana na sababu hiyo. 

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa Polisi George Kyando amesema vifo vinavyosababishwa na wivu wa mapenzi kwa mwaka huu vimeongezeka maradufu  ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.

Kamanda Kyando amesema idadi kubwa ya matukio hayo yanatekelezwa na wanaume na kwamba chanzo ni wanandoa  kutuhumiana kuhusu suala la uaminifu.

“Kipindi cha Januari hadi Oktoba 2021 kwa mkoa wa Shinyanga kumekuwa na ongezeko kubwa la mauaji yanayotokana na wivu wa mapenzi kwa mwaka huu jumla ya mauaji 12 yametokea ambayo chanzo chake  ni wivu wa mapenzi na kati ya hayo ni moja tu ambalo mwanamke alimuua mwanaume kwa wivu wa mapenzi na wengiwao wanawatuhumu wenzi wao kwamba siyo waminifu wa ndoa ambapo mwaka jana matukio kama haya yalikuwa 4 tu ya wivu wa mapenzi”. 

Hata hivyo kamanda Kyando amesema Mkoa wa Shinyanga umefanikiwa kukomesha mauaji ya vikongwe, albino na vifo vinavyosababishwa kulipiza kisasi.

Wakati huo huo kamanda Kyando amesema licha ya kupungua kwa matukio kama hayo lakini hali ya usalama katika Mkoa wa Shinyanga ni shwari ambapo ameonya pia kuelekea mwisho wa mwaka Jeshi hilo limejipanga kuhakikisha  hali ya amani, utulivu, usalama wa raia na mali zao inaendelea kuwepo. 

“Tabia ya matukio mbalimbali kuongezeka Jeshi la Polisi tumejipanga kukabiliana na hali hiyo hatutaruhusu hata kidogo tumejipanga kwa upande wa usalama barabarani hata kwa waharifu ambao wanategemea mwisho wa mwaka nawaonya wajue Jeshi la lao tukoimara hatutaruhusu matukio mabaya mkoa wetu ole atakae jaribu kitakachompata atakuwa fundisho kwa wengine waliokuwa na mawazo kama hayo”.

Kwa upande wake mchungaji wa kanisa la AICT Kambarage mjini Shinyanga Charles Lugembe amesema baadhi ya ndoa zinakuwa zikiteteleka kutokana na wahusika kutokuwa makini katika mahusiano yao. 

“Matokeo ya anguko la mwanadamu taasisi ya ndoa imekuwa ikishambuliwa sana hata wakristo katika kanisa wanashida hiyo jinsia au mapenzi yanapotumika vibaya lazima ugonvi, wivu, watoto nje ya ndoa  na mauaji yatokee haya yote ni matokeo ya dhambi na hii ni kwa sababu tu watu wameshindwa kujua matumizi mazuri na sahihi ya mapenzi”.

Mchungaji Lugembe amesema watu wanaoishi katika ndoa wanatakiwa  kuwa waaminifu,waadilifu na wenye kumshirikisha Mungu katika maisha yao, hali ambayo itachangia kuimarisha mahusiano yao na kudhibiti migogoro inayosababisha vifo pamoja na madhara mengine. 

Amewaasa wanandoa kuzingatia viapo na mafundisho  ya dini katika imani zao kwani ndiyo silaha ya kulinda na kuimarisha mahusiano katika ndoa. 

“Msaada mwingine kwa wanandoa ili wabaki katika nafasi nzuri ya mzunguko wa maisha ni kuheshimu viapo, viapo vinavyotolewa kanisani vinaweka mhuri katika moyo wa mtu sasa unapokiuka unatafuta mhuri mwingine tayari inaleta shida yakutokuaminika wivu wa Mungu unaweza kutufundisha namna ya kuwapenda wake zetu au waume zetu lazima uwe na wivu na hali ya kumpenda mke wako lakini wivu wa kumchukia ni mbaya na inapelekea vifo hivyo mke wako au mme wako ikitokea amekiuka basi uwepo msamaha kuombeana msamaha ni jambo la msingi kwa sababu msamaha unaweza kutoa hali ya mauaji”.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi katika Manispaa ya Shinyanga wamesema kuporomoka kwa maadili na jamii kukosa hofu ya Mungu ni moja ya sababu ambayo imekuwa ikisababisha migogoro baina ya wanandoa na badaye vifo vinavyotajwa kuwa chanzo chake ni wivu wa mapenzi.

Wananchi hao wameshauri kwamba ili kudhibiti vifo vinavyotajwa kusababishwa na wivu wa mapenzi ni wajibu wa wanandoa kuishi maisha ya uadilifu na kumshirikisha Mungu ili kujenga familia bora yenye amani, na upendo.