Mradi wa kuimarisha familia sos dar yaandaa mpango shirikishi kwa wadau wake

 

Na Mwandishi wetu

Mratibu wa mradi wa kuimarisha familia kutoka shirika la SOS Villages mkoa wa Dar es Salaam Kennedy Mashema amesema kuwa wanewekeza nguvu nyingi katika Vikundi vya CBO kwa lengo la kuweza kujisimamia wenyewe wanavikundi  katika miradi  walioanzisha.

Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dar es Salaam wakati alipokua katika kikao cha uchambuzi wa fursa mbalimbali kwa lengo la kuandaa mpango mkakati shirikishi wmbao umelenga kuona matunda ya mradi huo  endapo Kama shirika hilo litaondoka katika kata ya Chanika na Zingiziwa.

Amesema kuwa, lengo la kukutana kwao ni kuweza kuandaa mpango ambao utaviwezesha vikundi hivyo kuweza kujisimamia wenyewe katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo ikiwemo kujisimamia katika masuala ya ujasiriamali.

“Wameshaanza kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kusimamia miradi ya ujasiriamali ikiwemo mashamba darasa, kutembelea wagonjwa, kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, kwani tulianza kudili na chanzo cha tatizo la ukatili kwa kuanza kutoa semina kwa familia”amesema Kennedy.

Kwa upande wake, kiongozi wa kikundi cha Saut ya jamii Kipunguni Selemani Bishagazi, amesema kuwa wameamua kuungana na Shirika hilo kwa lengo la kuunganisha nguvu za pamoja katika mapambano ya ukatili wa kijinsia pamoja na kutoa msaada wa kisheria kwa wahanga wa vitendo vya ukatili.

“Lengo letu la kuungana na kwa pamoja na SOS ni  kutaka kutoa huduma kama tunazozitoa kule Kipunguni ikiwemo kuwafundisha namna bora ya kuweza kupambana na ukatili kwa kuwawezesha kiuchumi kwa kuwafundisha ujasiriamali pamoja na kuwapa fursa za kuwaunganisha na wafadhili mbalimbali”amesema Bishagazi.

Naye, Mwenyekiti wa CBO Sayari kutoka Kata ya Chanika na Zingiziwa Nipael Joshua amesema kuwa wamepata elimu ya kujitambua pamoja na kupata elimu ya kuanzisha mashamba darasa na kusimamia vikundi mbalimbali vya hisa (kukopa na kulipa).