Na Mwandishi Wetu, APC BLOG, ARUSHA
MKUFUNZI wa Chuo cha Ufundi cha Arusha (ATC) Lusato Kanyika anashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani hapa kwa madai ya kuomba rushwa ya ngono kutoka kwa mwanafunzi mmoja chuoni hapo ambaye jina lake linahifadhiwa.
Akizungumza chuoni hapo Afisa Habari wa ATC, Gasto Leseiyo alisema mwalimu huyo alikamatwa na maafisa wa TAKUKURU katika moja ya nyumba za kulala wageni (Guest House) Jijini hapa akiwa katika harakati za kufanya na ngono na mwanafunzi huyo.
Leseiyo alisema kuwa kwa mwalimu huyo anadaiwa kuomba ngono kutoka kwa mwanafunzi huyo kwa lengo la kumsadia kufaulu somo la mafunzo viwandani (IPT). Hata hivyo pia alidai kushangazwa na hatua ya mwalimu huyo kukumbwa na pepo la ngono wakati yeye ni mwokovu na anampenda yesu.
Alisema chuo hicho kimeshtushwa na taarifa hiyo ya rushwa ya ngono na itatoa ushirikiano kwa Takukuru endapo wakiitwa kuhojiwa kuhusiana na tuhuma anazokabiliwa Mwalimu huyo mlokole.
“Ni kweli tukio hili limetokea na tumeshindwa kuamini kama kweli yeye anahusika kutokana na ulokole alionao mwalimu huyo ila tuhuma ni tuhuma tu maana somo lenyewe hilo la viwandani ni somo ambalo kila mwanafunzi anafaulu kirahisi kwa kupata alama ya A+
Alisema chuo kinatoa pole kwa familia ya mwanafunzi huyo wa kike pamoja na wanafunzi chuoni hapo ijapokuwa bado chuo kinajiuliza kwanini mwanafunzi huyu wa kike alipoona anasumbuliwa na Mwalimu Kanyika hakutoa taarifa kwa kamati ya maadili ya shule au hata msimamizi wake.
“Ukiangalia Mwalimu mwenyewe ni mtu ameshika dini tunashangaa kwa tuhuma hizi za rushwa ya ngono,”alisema Lesioyo.
Akizungumzia tukio hilo Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani hapa, Frida Wikesi alikiri kuchunguza tuhuma hizo na kudai kuwa endapo ikidhibitika ni kweli mwalimu huyo aliomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi huyo watatoa taarifa rasmi
Hata hivyo alisema mwalimu huyo yupo nje kwa dhamana baada ya kukamatwa Agosti 2 mwaka huu baada ya kuwekewa mtego akiwa katika nyumba moja ya kulala wageni(Jina linahifadhiwa)jijini hapa.
Alisema jalada la kesi hiyo limepelekwa kwa mwanasheria wa Serikali kuandaliwa mashtaka na kwamba iwapo litarejea na kubainika mtuhumiwa ana kesi ya kujibu watamfikisha mahakamami muda wowote.