Na Mwandishi Wetu, Pemba
Mahakama ya Mkoa wa Chake chake Pemba imemuhukumu kutumikia chuo cha mafunzo (Jela) miaka 15, mwalimu wa Madrasa ya Mwambe Pemba, Alli Usi Simai baada ya kumkuta na hatia ya kumbaka mwanafunzi wake wa miaka 8.
Hukumu hiyo imetolewa jana na Hakimu Muumini Alli Juma, wa Mahakama hiyo maalum ya makosa ya udhalilishaji iliyoko katika Mkoa wa Chake chake Pemba.
Awali ilidaiwa Mahakamani hapo na Mwendesha mashtaka wa Serikali Ali Amour Makame kuwa mshtakiwa huyo alidaiwa kufanya kosa hilo Novemba 28, 2021 majira ya saa9. 00 alasiri huko Mchakwe Mwambe Wilaya ya mkoani mkoa wa kusini Pemba.
Mshtakiwa alikuwa na mashahidi wanafunzi watatu ambao pia ni wanafunzi wake chuoni hapo ambao katika ushahidi wao kwa pamoja walipinga mwalimu wao kutenda kosa hilo.
Kwa upande wa Serikali Idadi ya mashahidi ilikuwa watano ambao ni mtoto mwenyewe aliyebakwa, Daktari aliyemfanyia vipimo, wazazi wake pamoja na askari wa upelelezi ambao walitoa ushahidi wao mahakamani ulitosha kumtia hatiani mwalimu huyo bazazi.
Hakimu Muumini Ali juma bila ya kuwa na chembe ya shaka kutokana na ushahidi uliotolewa alikubaliana na upande wa mashtaka na kumuamuru mshtakiwa Ussi Simai kutumikia chuo cha mafunzo kwa kipindi cha miaka 15 ili iwe fundisho kwake na kwa wengine wenye tabia kama hiyo.