Naibu waziri kasekenya atoa siku 10 mizani ya nyakahura, kagera kukamilika

 

Naibu
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, akiongea na
wakazi wa kata ya Rulenge Wilayani Ngara, aliposimama kuzungumza nao
wakati akikagua barabara ya Omubuga, Rulenge hadi Murugarama (KM 32),
iliyotengewa fedha na Serikali kwa ajili ya kuanza kujengwa kwa kiwango
cha lami.Mbunge
wa Jimbo la Ngara Ndaisaba Ruhoro (mwenye suti ya bluu), akifafanua
jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya
(kushoto), wakati akikagua barabara ya Omubuga, Rulenge hadi Murugarama
(KM 32), iliyotengewa fedha na Serikali kwa ajili ya kuanza kujengwa kwa
kiwango cha lami. Kushoto kwa mbunge huyo ni Mkuu wa Wilaya ya Ngara
Col. Mathias Kahabi.Ukarabati
wa miundombinu ya mizani ya Nyakahura iliyoko wilaya ya Ngara mkoani
Kagera, ukiendelea kwa kasi. Mizani hiyo inatumika kupima magari makubwa
ya mizigo zaidi ya 400 kwa siku, yanayofanya safari zake kati ya
Tanzania, Burundi na Rwanda.Ujenzi
wa daraja la kudumu la Kitengule lenye urefu wa meta 140 ukiendelea.
Kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo kutaziunganisha wilaya za Karagwe
na Misenyi Mkoani KageraMeneja
wa Wakala wa barabara (TANROADS) mkoa wa Kagera Mhandisi Ntuli
Mwaikokesa, akimkumbusha jambo Mhandisi Mkazi Charles Romisha, wakati wa
ukaguzi wa ujenzi wa daraja la Kitengule na barabara unganishi (KM18).
Wa kwanza kulia ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey
Kasekenya, akifuatiwa na Mkuu wa Wilaya ya Karagwe.Naibu
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, akiongea na
waandishi wa habari (hawapo pichani), wakati akikagua ujenzi wa daraja
la Kitengule lenye urefu wa meta 140, na barabara unganishi (KM18),
kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Col. Sakulo akifuatiwa na
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Misenyi mkoani Kagera.


PICHA NA WUU


…….


Naibu
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ametoa siku
10 kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Kagera,
kuhakikisha anamsimamia mkandarasi anayejenga mizani ya Nyakahura
mkoani humo, kumaliza ujenzi na kuanza kutolewa huduma za upimaji wa
magari katika mizani hiyo kama zamani.


Akizungumza
katika ziara yake ya kukagua miradi ya barabara, mizani na madaraja
mkoani humo, Naibu Waziri Kasekenya, amesema kuwa kusimama kwa huduma za
upimaji wa magari katika mizani hiyo kunaisabibishia Serikali hasara
kubwa, kwani kupitia fursa hiyo magari yanaweza kuzidisha uzito na
kupelekea kuharibu barabara.


“Ujenzi
wa mizani hii inabidi ukamilike mapema iwezekanavyo, nimeambiwa hapa
kwa siku yanaweza kupita magari zaidi ya 500, hivyo magari kutokupima
hapa inaweza ikawa sababu ya wasafirishaji kuzidisha uzito na kupelekea
kuharibu barabara zetu ambapo Serikali inatumia kiasi kikubwa cha fedha
ili kuzijenga”, amesema Kasekenya.


Aidha,
amemuagiza Meneja huyo kufanya utaratibu wa kuandaa mchoro wa mizani
nyingine ya pili, pembezoni mwa mizani ya kwanza ili kuepusha msongamano
amabao unaweza kujitokeza.


“Haiwezekani
sehemu inayopitisha magari mengi kama hii ikawa na mizani moja ya
kupima magari yanayotoka na yanayoingia nchini, hivyo nakuagiza tena
Meneja kuandaa mchoro na kuuwasilisha Wizarani ili tutenge fedha kwa
ajili ya mizani ya pili”, amesisitiza Kasekenya.


Kuhusu
suala la barabara katika mkoa huo, Kasekenya amesema kuwa Serikali
imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 12.8 kwa ajili ya ukarabati mdogo wa
barabara ya Lusahunga – Rusumo (Km 92), huku ikisubiri taratibu za
manunuzi ya kumpata mkandarasi wa kufanya ukarabati mkubwa.


Katika
hatua nyingine, Naibu Waziri Kasekenya, amekagua daraja la Kitengule
lenye urefu wa mita 140 na barabara za maingilio zenye urefu wa kilometa
18 ambapo ameridhishwa na kasi ya ujenzi ya mradi huo unaojengwa na
mkandarasi M/s China Henan.


Amebainisha
kuwa daraja hilo ambalo linaunganisha wilaya ya Karagwe na Misenyi,
litakuwa ni njia ya mkato kati ya wilaya hizo mbili na hivyo kurahisisha
huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa wilaya hizo na
mwekezaji wa kiwanda cha sukari kwa ujumla.


Kwa
upande wake, Mbunge wa jimbo la Ngara, Mheshimiwa Ndaisaba Ruhoro,
ameipongeza Serikali kwa kutoa shilingi Bilioni 6 kwa ajili ya
maandalizi ya kuanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami za
Nyakahura – Kumubuga – Murusugamba (Km 75), Kumubuga – Rulenge –
Mururama (Km 32) na Rulenge – Kabanga Nickel (Km 34) ambapo amesema kuwa
kukamilika kwa barabara hizo kutarahisisha huduma za usafiri na
usafirishaji kutoka wilaya hiyo kuelekea wilaya jirani na hata nchi
jirani za Rwanda na Burundi.


Naye,
Msimamizi wa Daraja la Kitengule, Charles Rumisha, amesema kuwa mradi
ulianza mwezi Oktoba, 2018 na kutarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka
huu ambapo amesisitiza kuwa mpaka sasa wamefika katika hatua nzuri.


Amefafanua
kuwa kwenye upande wa barabara ujenzi umefika asilimia 88 na kwa upande
wa daraja mkandarasi tayari keshakamilisha ujenzi wa nguzo zote nne,
kilichobaki ni kuweka usawa wa juu wa barabara.


Naibu
Waziri Kasekenya, yupo katika ziara ya siku Tatu mkoani Kagera ambapo
atakagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na na Wizara hiyo ili kujionea
maendeleo yake.