Naibu waziri katambi akabidhi shivyawata msaada wa vifaa saidizi

 Na  Mapuli Misalaba,  Shinyanga

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi  leo amekabidhi msaada wa vifaa saidizi kwa Shirikisho la Vyama vya watu wenye ulemavu SHIVYAWATA Mkoa wa  Shinyanga.

Katambi ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini amekabidhi  Baiskeli 10 zenye magurudumu matatu za watu wenye ulemavu wa viungo, fimbo nyeupe 60 kwa ajili ya wasioona pamoja na magongo 60 ya kutembelea wenye ulemavu

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo amesema serikali ya Rais SAMIA SULUHU HASSAN, inatambua na kuthamini makundi yote wakiwemo watu wenye ulemavu na kwamba wataendelea kupata huduma bora na stahiki kadri ya mahitaji yao

“Ndugu washiriki serikali yenu chini ya uongozi shupavu na thabiti kabisa na usimamizi wa mama Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawajali sana wanawake wote na inatambua uwepo wa makundi mbalimbali katika jamii yakiwemo makundi ya watu wenye ulemavu ambalo ni kundu muhimu ambalo mheshimiwa Rais kwa maelekezo yake kwake sisi wasaidizi ametuelekeza lazima tuyaguse makundi haya muhimu na nilazima tutafute namna ya kuweza kuwasaidia”

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu Mkoani Shinyanga (SHIVYAWATA) MOHAMED ALLY, amempongeza mbunge Katambi kwa msaada wa vifaa hivyo saidizi, ambapo amesema vitawasaidia kufika maeneo mbalimbali, wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

“Mapokezi ya hivi vifaa vya uwezeshi ninashukuru sana vitatusaidia kwa namna moja au nyingine na hali ya mtu mwenye ulemavu ninauhakika sasa hivi atafika kazini kwa wepesi na kufanya shughuli zake kwa uhuru zaidi kuliko zile za kubebwa bebwa nazani hii itasaidia zaidi”