Naibu waziri maliasili na utalii mhe. mary masanja afanya ziara expo 2020 dubai*

 

Na Abubakari W Kafumba, UAE

Juzi  13 Desemba 2021 Mhe. Balozi Mohamed Mtonga Kamishna Jenerali wa Banda la Tanzania na Bi. Getrude Ng’weshemi kutoka TanTrade, Mkurugenzi wa banda hilo katika Maonesho ya Expo 2020 Dubai wamemkaribisha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Francis Masanja aliyeambatana na Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Edwin Rutageruka.

Mara alipowasilili, Mhe. Mary Masanja alikaa kikao na watumishi wanaowakilisha Taasisi za Sekta mbalimbali zinazoshiriki kwenye Maonesho ya Dunia ya Expo 2020 Dubai ambapo alipokea taarifa iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Banda la Tanzania Bi. Getrude Ng’weshemi inayoeleza ushiriki wa Tanzania kwenye maonesho ya Expo 2020 Dubai ikiainisha mafanikio yaliyopatikana na hatua zinazochukuliwa katika kuhakikisha ushiriki unaendelea kuwa wa uhakika na wenye tija.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii na Kamishna wa Uhifadhi TANAPA Dkt. Allan Kijazi na Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara wa TANAPA Bw. William Mwakilema na watumishi wanaoshiriki katika maonyesho haya kutoka Taasisi za Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS). 

Baada ya kupokea taarifa hiyo Mhe. Mary Masanja alionyesha kufarijika na hatua ambayo imefikiwa mapaka sasa tangu maonesho haya yaanze rasmi tarehe 01 Oktoba 2021. Amesema, ‘’Nawapongeza wote kwa jitihada zenu za kuendelea kusukuma gurudumu hili, muendelee kuiwakilisha vema Tanzania hapa Dubai. Kwa sasa hii ndio sehemu yenye mkusanyiko mkubwa ambapo mataifa 192 kutoka maeneo mbalimbali Duniani yanakutana. Tuituie vizuri fursa hii kuhakikisha tunaitoa nchi yetu kimasomaso”.

Aidha Mhe. Mary Masanja amechukua nafasi hiyo pia kuwahimiza Taasisi zilizo chini ya Sekta ya Utalii na wadau wake kuchangamkia fursa kwa kushiriki kwenye maonyesho haya kwa malengo na kuhakikisha kuwa Sekta ya Utalii inaitangaza Tanzania kwa uhakika ili hatimaye ulimwengu mzima uweze kufahamu jinsi nchi yetu imebarikiwa na rasilimali za kipekee na kuonyesha fursa zinazoiweka Tanzania mbele katika maendeleo ya kisekta unapoongelea Sekta ya Utalii Duniani.

Baada ya kumaliza kikao hicho, Mhe. Mary Masanja pamoja na viongozi wengine alioambatana nao waliongozwa na Mkurugenzi wa Banda la Tanzania Bi. Getrude Ng’weshemi kutembelea banda ambapo  waliweza kujionea maudhui ya vipaumbele yanayoitangaza Tanzania kwenye maonesho ya Expo 2020 Dubai. Asilimia kubwa ya maudhui kwenye banda  ni yanayoitangaza Tanzania kupitia Sekta za Utalii, Madini, Kilimo, Nishati, Utamaduni, Viwanda na Uwekezaji.

Vilevile Mhe. Mary Masanja na viongozi alioambatana walipata nafasi ya kutembelea mabanda ya nchi za Afrika Mashariki za Kenya na Rwanda pamoja mabanda mengine ya nchi za Kuwait na Qatar. Lengo lilikuwa ni kujifunza kutoka nchi hizo na kupata uzoefu wao wa kushiriki kwenye maonesho makubwa ulimweguni kama haya.

Fursa ya kuwa sehemu ya maonyesho haya ni ya kipekee na yenye manufaa kwa Tanzania na watanzania na ni sehemu na nafasi nzuri ya kujifunza, kupata uzoefu, kujitangaza na kukuchochea maendeleo ya Sekta mbalimbali nchini kupitia fursa za ushirikiano na nchi mbalimbali. 

Ushiriki huu unategemewa kuleta hamasa kubwa na kuchochea ukuaji na maendeleo ya Sekta mbalimbali kupitia mafanikio ya ushiriki we Tanzania kwenye maonyesho haya ikiwemo uwekezaji wa kisekta na ushirikiano endelevu baina ya Tanzania na mataifa mengine ulimwenguni.