Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Mh Anthony Mavunde amewataka
waajiri wote wanaoleta wafanyakazi wa Kigeni kuhakikisha wanasimamia na
kutekeleza mpango wa urithishaji ujuzi kwa Wafanyakazi wazawa kama
inavyolekezwa na Sheria ya Uratibu ya Ajira kwa Wageni Na. 1 ya Mwaka
2015.
Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Jijini Dar es salaam katika ofisi za
makao mkuu ya Kampuni ya Magari ya TATA wakati wa uzinduzi wa Program ya
Kukuza Ujuzi kwa Vijana inayojulikana kama SkillPro ambayo Vijana
mafundi wa Kitanzania wanapata nafasi ya kupata ujuzi Nchini India namna
ya kutengeneza Magari aina ya TATA na ufundi wa Jumla wa magari,pamoja
na uzinduzi wa Gari ambalo ni Gereji inayotembea itakayopita kwenye
gereji za mtaan kuwafundisha mafundi na kuwatambua kwa kuwapa vyeti vya
kutengeneza magari ya TATA.
“Nawapongeza
TATA kwa mpango huu wa kuwajengea ujuzi Wafanyakazi wazawa,Waajiri
wengine waige mfano huu wa kuja na program zenye nia ya kurithisha ujuzi
kwa wafanyakazi ili kupunguza utegemezi wa wafanyakazi kutoka nje ya
nchi.Wale waajiri wenye wafanyakazi wageni na hawatekelezi mpango wa
urithishaji wa Ujuzi kwa mujibu wa sheria,hatua stahiki zitachukuliwa
dhidi yao kwa kukiuka utaratibu wa sheria”Alisema Mavunde
Mkurugenzi Mkuu wa TATA, Ndg Rajiv Bhushan ameeleza bayana kwamba
Kampuni yake imejipanga kuwawezesha Vijana wa kitanzania kwa kutekeleza
program mbalimbali za mafunzo ya Ufundi na kuonesha utayari wa
kushirikiana na serikali kutatua changamoto ya ukosefu ya ujuzi stahiki.
kwa niaba ya wanufaika wa Program hii,Ndg Osmund Kapinga amepongeza
mafunzo yanayoendeshwa na Kampuni hii ya TATA nchini India ambayo
yanawafanya kupata ujuzi wa ziada tofauti na ufundi hali ambayo
imepelekea kupata nafasi za utawala ambapo amejitolea mfano yeye
mwenyewe kwa kuteuliwa kuwa Meneja wa Tawi la TATA Arusha.