Nssf washauriwa kusajili wanachama wasio kwenye sekta rasmi nchini

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Said Mtanda

 

Na Mwadishi wetu,Arusha 

Mfuko wa Taifa wa hifadhi ya Jamii(NSSF) umetakiwa kujikita zaidi kusajiri wanachama wapya kutoka sekta zisizo rasmi  ili kupata wanachama wengi wa kujiunga na mfuko huo na kuacha kutegemea sekta rasmi pekee.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa wilaya ya Arusha, Saidi Mtanda wakati alipokuwa akifungua semina ya waajiri ambao ni wanachama wa mfuko wa NSSF Mkoa wa Arusha na kuwasisitiza waajiri hao kuhakikisha wanawasilisha makato ya wafanyakazi wao Kwa wakati katika mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Mtanda ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Arusha ,John Mongela akibainisha kwamba sekta zisizo rasmi kama kundi la Machinga na Dereva bodaboda ni muhimu Sana Kwa Sasa kuwapatia elimu ili waweze kuhamasika kujiunga na mfuko huo.

“Hamasisheni sekta zisizo rasmi ili kwa kuwapatia vijana elimu waweze kujiunga na mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwani zipo faida nyingi za kuwanufaisha wanapokuwa wanachama ikiwemo kupatiwa bima Kwa ajili ya matibabu Bure”alisema.

Aidha mkuu huyo wa wilaya alitoa wito Kwa mfuko huo wa NSSF kuhakikisha inalipa mafao ya wanachama wao Kwa wakati na kuacha usumbufu usio na tija unaosababisha baadhi ya wazee kukata tamaa na wengine kufariki dunia wakifuatilia mafao yao.

Katika hatua nyingine Mtanda aliutaka mfuko huo kutosita kuwafikishia mahakamani waajiri wakorofi wasiotaka kufikisha michango ya wanachama licha ya kwamba wamekuwa wakiwakata fedha za kuchangia.

Awali meneja wa NSSF Mkoa wa Arusha,Josephat Komba alisema mfuko huo upo katika hatua ya kuhakiki wanachama wake na kusajiri wanachama wapya kupitia sekta zisizo rasmi  na wameanza kuboresha skimu ya sekta isiyo rasmi na hivi karibuni wataanza kampeni ya kutoa elimu kwa sekta hiyo.

Alisema semina hiyo imelenga kuwakumbusha waajiri wajibu wao na watatambulisha pia mfumo mpya wa tehama utakao mwezesha mwajiri kusajili. mwanachama na kulipa michango yao kirahisi akiwa ofisini kwake bila kumlazimu kwenda ofisi za NSSF  .

Aidha alisema kuwa NSSF  imekuwa na utaratibu wa kuchukua hatua waajiri wasiowasilisha  michango ya wanachama  kama sheria inavyosema.

Katika hatua nyingine mkurugenzi huyo alisema kuwa mfuko huo ulichukua hatua ya  kutoa msamaha Kwa waajiri wote wenye malimbikizo ya madeni yanayoishia juni 2021 kwa kuwapunguzia mzigo wa  tozo.

“Kama waajiri wote wangelipa malimbikizo yao ndani ya mwezi wa 11,12 na Januari 2022 wangepatiwa msamaha wa tozo, hivyo wito wangu Kwa waajiri ni kuhakikisha wanawasajiri wafanyakazi wao kwenye mfuko na kuwasilisha makato yao Kwa wakati kama sheria inavyoelekeza nanhii itasaidia kuondoa usumbufu wakati mfuko unataka kuwalipa mafao yao “alisema.