Oxfam, wadau wakutana shinyanga kujadili namna ya kukabiliana na maafa

 Na Mapuli Misalaba,SHINYANGA

Shirika la Oxfam kwa kushirikiana na kamati ya maafa wamefanya kikao kujadili namna bora ya kukabiliana na majanga mbalimbali yanayosababisha maafa.

 Kikao hicho kilichoratibiwa na shirika la Oxfam kimehusisha baadhi ya asasi za kiraia ikiwemo shirika la Redeso, Rudi, viongozi wa serikali ngazi ya mkoa na wilaya pamoja na maafisa watendaji wa kata na vijiji

Mratibu wa miradi ya shirika la oxfam kanda ya  mwanza Velentine Shipuya ametaja lengo la kikao hicho kuwa  ni kuangalia namna bora ya uratibu wa shughuli za kupunguza athari za maafa pamoja na ukatili wa kijinsia.

“Kwa ujumla leo tumekutana hapa na wadau kwa ajili ya kuangalia namna bora zaidi ya kufanya huu uratibu wa shughuli za kupunguza athari za maafa kama tunavyofahamu mradi huu unaelekea mwisho tunategemea kukamilisha mwaka huu mwezi wa 12 sasa tunavyoumaliza huu mradi hao wadau wengine wanauendelezaje ndio maana tuko hapa kwenye kikao ambacho kinahusisha wadau wote wa kamati ya maafa ngazi ya kata, wilaya na ngazi za Mkoa kwa ujumla wake”amesema Shipuya

Amesema miradi ya maafa inamalizika mwezi wa 12 mwaka huu na kuiomba serikali kuendeleza mazuri ambayo yameonekana ili kuendeleza amani, upendo na ushirikiano katika jamii.

“Tunapoende kuishia mwezi wa 12 basi serikali ichukue yale  matokeo mazuri ambayo yameonekana kutokana na huu mradi serikali iyaendeleze itakuwa jambo la heri kabisa itaweza kuwafikia wengi zaidi maana sisi hatujawafikia wananchi wote tumefika baadhi ya vijiji lakini bado kuna vijiji vinauhitaji”amesema Shipuya.

Akifungua kikao hicho kwa niaba ya katibu wa mkoa wa Shinyanga, katibu tawala msaidizi uchumi na uzalishaji Mkoa wa Shinyanga  Beda Chamatata amesema ni vyema kamati ya maafa kujiweka tayari kila wakati ili kukabiliana na maafa pale yanapojitokeza.

“Kama tunavyofahamu maafa siyo kitu ambacho kinatokea mara kwa mara mara vyingi kinatokea ghafla sasa tunaposhirikishana ngazi ya kata, wilaya na Mkoa tunapaswa majukumu yetu tuyatekeleze kwa ufasaha zaidi wakati yanapotokea majanga kama hatujapangana vizuri tunaweza tukakwama kwahiyo ni muhimu tupange kwamba tutumie njia ipi ya kuwasiliana ili iwe rahisi kufika kwenye tukio kabla uharibifu mkubwa haujatokea”amesema chamatata

Kwa upande wake mratibu wa miradi ya shirika la Redeso linaloshugulika na mradi wa kupunguza athari za maafa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu Charles Boraga amesema wilaya hiyo  inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mafuriko na ukame pamoja na ukatili wa kijinsia  na mimba za utotoni

“Changamoto iliyopo kwa upande wa Kishapu eneo la ukanda wa utilima kijiji ukoma mwamala wao wanachangamoto ya ukame lakini baada ya muda wanakuwa na changamoto ya mafuriko lakini pia kuna ukatili wa kijinsia pamoja na mimba za utotoni bado ni changamoto”

Naye kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu Sigsbert   Rwezaka amelipongeza shirika la Redeso kwa kuwapatia elimu na mafunzo ya kuepuka  ukatili pamoja na  majanga mbalimbali  yaliyokuwa yakitokea kwa  wananchi wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu .