Polepole: rais magufuli hataongeza hata dakika tano muda wake wa uongozi ukiisha


Na Mwandishi Wetu, APCBLOG, DODOMA 

KATIBU wa Itikadi na unenezi wa Chama cha mapinduzi (CCM) Humphrey Polepole amesema kuwa ametumwa na Mwenyekiti wa chama hicho ambaye pia ni Rais wa Tanzania Dr. John Magufuli awaeleze watanzania wote kuwa hayupo tayari kuendelea kuongoza nchi mara baada ya muda wake wa uongozi kufika kikomo kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakitaka iwe hivyo.

Polepole amezungumza hayo  jana akiwa mkoani Dodoma wakati akizungumza na baraza kuu la umoja wa wanawake wa chama hicho (UWT) ambapo amewataka wanachama hao kuacha kuendeleza mjadala huo ambao Mwenyekiti wao amesema unamkwaza.


Kwa mujibu wa Polepole, aliitwa na Mwenyekiti wa CCM Rais Magufuli na kumtaka awatangazie Watanzania kwamba nchi inaongozwa na katiba na sheria.

Alisema Rais alisikia watu wakizungumza kuhusu kuongezewa muda baada ya kumaliza ukomo wa muda wa uongozi wake na kusema ni jambo linalomkwaza.

Alisema muda wake wa kumaliza uongozi ukifika mwisho atang’atuka mara moja na hataongeza hata dakika tano kwa kuwa uongozi ni mgumu.

“Wale wanachama wenzangu ambao mnaendeleza huu mjadala wa kuongezwa muda wa uongozi naomba muuwache maana Mwenyekiti anasema anakwazwa,”alisema Polepole.

Kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa, aliwataka katika kuteua wagombea wajiepushe na walaghai na wasio kubalika na jamii kwa kuwa inawavunja moyo wanawake ambao ni wapiga kura waaminifu.

“Wapiga kura waaminifu ni wanawake lakini tungesema wanaume wakapige kura tungeshaliwa kitambo. Tusiwavunje moyo wanawake kwa kuwateulia wagombea wasio na uwezo,”alisema.

Sambamba na hilo, Katibu alisisitiza kuendelea kuwatumia wanawake kwenye nafasi mbalimbali za uongozi kwa kuwa watalisaidia taifa kupiga hatua zaidi kimaendeleo.