Prf kabudi ahudhuria mkutano wa mawaziri wa ticad jijini yokohama japan


Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe.Kono Taro (mwenye tai ya rangi ya chungwa) akifungua rasmi Mkutano wa Mawaziri wa maandalizi ya Mkutano wa Saba wa Kimataifa kuhusu Mandeleo ya Afrika (TICAD 7) . Ufunguzi huo umefanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Pacifico jijini Yokohama, Japan tarehe 27 Agosti 2019.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (wa tatu kushoto kwenye meza nyeupe) akifuatilia ufunguzi wa Mkutano wa TICAD wa Mawaziri uliofanyika Yokohama, Japan tarehe 27 Agosti 2019


Mkutano ukiendelea

MKUTANO WA MAWAZIRI WA MAANDALIZI YA MKUTANO WA SABA WA TOKYO KUHUSU MAENDELEO YA AFRIKA (TICAD 7) WAFANYIKA JIJINI YOKOHAMA, JAPAN

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi leo tarehe 27 Agosti 2019 ameshiriki Mkutano wa Mawaziri wa Maandalizi ya Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Pacifico jijini Yokohama, Japan.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine unatarajiwa kupitia na kupitisha rasimu ya Azimio la Yokohama na Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Azimio hilo litakalowasilishwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utakaoanza tarehe 28 hadi 30 Agosti 2019 kwa ajili ya kuridhiwa.

Akifungungua mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe. Kono Taro amezipongeza nchi za Afrika kwa kupiga hatua katika maendeleo kupitia ushirikiano na Japan na kwamba nchi yake itaendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na nchi hizo ili kuziwezesha kufikia malengo ikiwemo mapinduzi ya viwanda.

Mhe. Taro alisema kuwa, ushirikiano kati ya Afrika na Japan kupitia mpango wa TICAD umeendelea kuimarika tangu kuanzishwa kwa mpango huo mwaka 1993 na kwamba ni matarajio yake Mkutano wa Saba utakuwa wa tija zaidi kwa pande hizo mbili.

“Nawakaribisha Mawaziri wenzangu Yokohama ambapo maandalizi ya mkutano wa saba wa kimataifa wa Tokyo kuhusu maendeleo ya Afrika yanaendelea. Jukumu letu ni kupitia na kupitisha rasimu ya Azimio la Yokohama na Mpango kazi wake ili hatimaye litunufaishe sote pale litakapopitishwa na Wakuu wa nchi” alisema Mhe. Taro.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano huo, Mhe. Sameh Shoukry ameipongeza Japan kwa kuendelea kuandaa mikutano hiyo ambayo ina nia ya kuifikisha Afrika katika mapinduzi ya viwanda na kuondokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana na umaskini.

Kwa upande wake, Naibu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ambao ni miongoni mwa waandaaji wa Mkutano wa Saba wa TICAD, Bw. Kwesi Quartey amesema kuwa, mkutano huo unafanyika wakati Umoja wa Afrika unaendelea kutekeleza agenda 2063. Agenda hiyo pamoja na mambo mengine inalenga kuziwezesha nchi za Afrika kufikia maendeleo ya hali ya juu kwenye sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu, teknolojia na miundombinu.

Kadhalika Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma za Kanda ya Afrika kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika, Bw. Lamin Manneh alisema kuwa ushirikiano kati ya Afrika na Japan kupitia TICAD umekuwa na mchango mkubwa kwenye maendeleo ya Bara la Afrika. Aliongeza kuwsema kuwa, Shirika lake ambalo linasimamia maendeleo linaridhishwa na ushirikiano uliopo kati ya Japan na Afrika ambao kwa kiasi kikubwa umefanikiwa.

Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Ushirikiano na Afrika pamoja na mambo mengine unatoa fursa ya kupanga mikakati ya ushirikiano na agenda za kimaendeleo zitakazotelezwa kati ya Japan na Afrika kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kuanzia mwaka 2019 hadi 2021.

Agenda za mkutano wa mwaka huu zinalenga kujadili mageuzi ya kiuchumi na kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kukuza sekta na uvumbuzi. Pia kuimarisha usalama na ustahimilivu endelevu kwenye jamii pamoja na kuendeleza jitihada za kuimarisha amani na usalama barani Afrika. Agenda za Mkutano wa Saba zinaenda sambamba na agenda 2063 ya Umoja wa Afrika, Agenda 2030 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa na maazimio mengine ya kimataifa kama Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa.

Mkutano huu ambao umewashirikisha Mawaziri kutoka nchi za Afrika, na wadau mbalimbali wa maendeleo unafanyika ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utakaofanyika kuanzia tarehe 28 hadi 30 Agosti 2019.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Yokohama, Japan.
27 Agosti 2019.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *