Prf. kabudi asisitiza mshikamano imara sadc kwa maslahi ya wananchi.


Na Mwandishi Wetu, APC BLOG, Dar es salaam 
MWENYEKITI Mpya wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, Prof. Palamagamba Kabudi amezitaka Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuendelea kushikamana katika Umoja na Mshikamano baina yao ili kujenga Uchumi imara na kuleta Maendeleo ya wananchi wake.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa nafasi hiyo leo Jijini Dar es Salaam, Prof. Kabudi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, alisema wakati umefika kwa Nchi za SADC kuungana pamoja katika kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika taasisi mbalimbali za kikanda na kujenga msingi imara wa ushirikiano.

Prof. Kabudi alisema kwa miaka mingi Nchi za SADC zimekuwa na ushirikiano mkubwa baina yao hivyo wakati umefika kwa wananchi wa Mataifa hayo kushuhudia manufaa ya ushirikiano huo yakileta manufaa makubwa katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.

Aliongeza kuwa Tanzania kwa upande wake imeendelea kuwa nchi rafiki na mshirika wa karibu kwa mataifa yote ya SADC kama inavyojidhihirisha katika historia ya mapambano ya uhuru wa Nchi nyingi za Kusini mwa Afrika, ambapo mataifa mbalimbali yaliweka kambi kwa ajili ya wapigania uhuru wake katika harakati zao za kudai uhuru kutoka kwa wakoloni.

“Mwaka huu tunatimiza miaka 20 tangu kufariki wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Kiongozi shupavu aliyejitoa pamoja na viongozi wengine wa SADC katika kupigania harakati za ukombozi wa Afrika, tunapaswa kumuenzi kwa kuhakikisha tunaimarisha umoja na ushirikiano uliopo kwa maslahi ya wananchi wetu” alisem Prof. Kabudi.

Prof. Kabudi aliwataka Viongozi wa SADC kuimarisha Umoja kwa kuwa ndiyo silaha kubwa ya ushindi katika kujenga mazingira bora ya uwekezaji na biashara ndani ya Nchi za SADC pamoja na kutoa ushirikiano wa karibu zaidi kwa sekta binafsi kwa ajili ya kuibua na kujenga fursa za uchumi jumuishi.

Naye Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stegomena Tax alisema jumuiya hiyo imekuwa ikitekeleza programu na miradi mbalimbali ya ushirikiano wa kikanda ndani ya jumuiya hiyo ambayo tayari imeleta mafanikio makubwa kupitia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Jumuiya hiyo ambao umeweza kutumia rasilimali mbalimbali ikiwemo madini na nishati kwa ajili ya kujenga uchumi jumuishi.

Anaongeza kuwa katika Mkutano huo wa 39 unaotarajiwa kuhitimishwa na Mkutano Mkuu wa Marais wa Nchi za Jumuiya hiyo tarehe 17-18 Agosti mwaka huu, Sekretarieti ya Baraza hilo imeweza kuzindua Baraza la Biashara la SADC ambalo litakuwa chachu ya kuunganisha sekta binafsi na ile ya umma katika kujenga uchumi jumuishi kupitia ajenda ya viwanda pamoja na usimamizi wa rasilimali mbalimbali ndani ya jumuiya hiyo.

Akizungumzia kuhusu majanga ya kibinadamu ndani ya SADC. Dkt. Tax alisema kati ya Mwezi Machi-April Jumuiya hiyo ilipata majanga ya kibinadamu katika Nchi za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe, ambapo pamoja na changamoto hiyo Wakuu wa Jumuiya hiyo waliungana pamoja na kuweza kuzisadia nchi hizo kwa kutoa misaada mbalimbali ya kibinadamu ikiwemo madawa na vyakula.

Kwa upande Mwenyekiti wa Baraza hilo anayemaliza muda wake, ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Netumbo Ndaitwah alisema Umoja na mshikamano wa Jumuiya hiyo umeendelea kuimarika kwa kuwa nchi nyingi zimeendelea kuwa katika hali ya umoja, amani na utulivu.