Na Seif Mangwangi, Arusha
MFUKO wa hifadhi ya Jamii (PSSSF) umeanza kulipa mafao waajiriwa walioondolewa kazini kwa kubainika kuwa na vyeti feki ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alilotoa hivi karibuni.
Hivi karibuni Rais Samia aliwataka watendaji wa mifuko ya hifadhi ya Jamii nchini kuwalipa mafao wafanyakazi wote waliopoteza ajira zao baada ya kugundulika kuwa na vyeti feki, zoezi ambalo lilifanywa katika serikali ya awamu ya tano.
Hilda Kinabo, Mwandishi wa habari wa kituo cha Radio5 akiuliza swali katika kikao hicho |
Akizungumza wakati wa kikao kazi na wanachama wa klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Arusha leo Ijumaa, Desemba 2, 2022, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama wa mfuko wa PSSSF, James Mlowe amesema tayari mfuko huo umewalipa wanachama 750 waliokumbwa na sakata la vyeti “feki”, baada ya kuwasilisha madai yao na nyaraka stahiki.
zoezi la kuwalipa mafao watumishi hao lilianza Novemba 1, 2022 na kwamba mfuko umejipanga kuhakikisha wote wanaostahili kupata mafao yao wanapata kwa wakati na litakuwa ni zoezi endelevu.
“PSSSF tumeitikia agizo la Mheshimiwa Rais, tumeanza kulipa wadai wa vyeti feki mafao yao na zoezi linaendelea vizuri sana, Wanachama waliopo katika orodha ya serikali na PSSSF ni 9,771 ambao wanadai malipo ya takribani shilingi bilioni 22.22.” Alifafanua.
Amesema amewataka watu wote waliokumbwa na kadhia ya vyeti feki wapeleke madai yao katika ofisi yoyote ya PSSSF iliyo karibu na madai yao yatafanyiwa kazi haraka sana, na kutoa tahadhari kuwa madai feki yatachunguzwa na watakaobainika hatua kali zitachukuliwa.
Waandishi wa Habari wanachama wa Klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Arusha wakimsikiliza meneja mahusiano na Elimu wa mfuko wa hifadhi ya jamii wa PSSSF James Mlowe(hayupo pichani) |
Akizungumzia madhumuni ya kikao hicho na wanachama wa klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Arusha, Mlowe amesema “lengo ni kutoa ufafanuzi juu ya utekelezaji wa majukumu ya Mfuko pamoja na kuendeleza uhusiano mzuri uliopo kati ya Mfuko na wanahabari wa Arusha”.
Mambo mengine aliyozungumzia , Mlowe ni pamoja na Malipo ya Mafao na Pensheni, Uwekezaji, Thamani ya Mfuko pamoja na mafanikio ambayo PSSSF imeyapata tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018 baada ya kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii ya PSPF, PPF,LAPF na GEPF.
“ Kila mwezi PSSSF inaingiza kwenye mzunguko zaidi ya shilingi bilioni 180 ikijumuisha malipo ya pensheni ya mwezi zaidi ya shilingi bilioni 60 zinazolipwa kwa wastaafu 158,000 pamoja na Mafao mengine zaidi ya shilingi bilioni 120,” alibainisha.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wanachama wa klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Arusha, Mratibu wa Klabu hiyo, Seif Mangwangi ameushukuru mfuko wa PSSSF kwa hatua yake ya kuendeleza mahusiano na waandishi wa habari nchini na kupongeza kazi nzuri ambayo imekuwa ikifanywa na mfuko huo.
Mwandishi wa habari wa magazeti ya The guardian na Nipashe Mkoa wa Arusha Allan Isack akiuliza swali katika kikao hicho |
>Amesema kwa maelezo ambayo yametolewa na Meneja uhusiano na elimu kwa wanachama wa mfuko wa PSSSF James Mlowe ni wazi malengo ya mfuko ni kutumikia wanachama wake na kuhakikisha wanafaidika na mfuko huo pindi wanapostaafu.