Rais museveni aingilia kati maandamano ya wanafunzi wa makerere….ayaagiza majeshi kuondoka chuoni mara moja

Rais
wa Uganda, Yoweri Museveni ameagiza wanajeshi wanaozingira chuo kikuu
cha Makerere kwa lengo la kutuliza maandamano waondoke mara moja chuoni
hapo kwani hiyo sio kazi yao na badala yake jeshi la polisi lisimamie
ulinzi chuoni hapo.


Wiki
iliyopita, Wanafunzi 15 walikamatwa na Polisi kwa kuchochea vurugu na
maandamano wakipinga ongezeko la asilimia 15 ya karo chuoni hapo.

Kwenye
maandamano hayo wanafunzi hao walichoma vituo viwili vya Polisi mjini
Kampala, Jambo lililopelekea Jeshi liingilie kati ili kutuliza ghasia
hizo.

Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa mapema wiki hii na Afisa Habari wa Rais
Museveni, Don Wanyama amesema kuwa Museveni ameagiza Wanajeshi waondoke
chuoni hapo na jukumu hilo lichukuliwe na Jeshi polisi.

“Rais
Museveni kasema wadau na viongozi wa chuo cha Makerere wakae chini
kujadili matatizo yanayoendelea katika chuo hicho. Asubuhi hii amempigia
Mkuu wa Chuo kamwambia wakae na wenzao wajadiliane. Pia ameagiza
Wanajeshi waondoke chuoni hapo na kazi hiyo iwe chini ya Jeshi la Polisi
la Uganda,”amesema Wanyama.

Mpaka sasa hatma ya ongezeko la ada chuoni hapo bado haijapatikana, Lakini hali ya usalama imeanza kurejea.

Ongezeko
la 15% liliidhinishwa na baraza la vyuo vikuu nchini Uganda, Wanafunzi
wanatakiwa kuanza kulipa ada yenye ongezeko hilo kwa miaka mitano ijayo
baadaye kila mwanafunzi atatakiwa kulipa 75% zaidi.