Mwandishi Wetu, Bukoba
Akiwa ziarani Bukoba, mkoa Kagera, Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali yake sasa itatoa ruzuku ya mafuta Shilingi bilioni 100 kila mwezi hadi kieleweke.
Rais Samia ameagiza ruzuku ya Shilingi bilioni 100 itolewe kwenye bajeti ya matumizi ya kawaida ya serikali (recurrent expenditure) kila mwezi kuanzia Juni mwaka huu hadi hapo bei za mafuta katika soko la dunia zitulie.
Maamuzi haya magumu na ya kishujaa ya serikali kujibana kwenye matumizi yake ili ipatikane ruzuku hiyo tayari yamesababisha bei za mafuta nchini ziteremke kuanzia Juni 1.
Ikumbukwe kuwa matumizi ya maendeleo ya bajeti ya serikali (recurrent expenditure) hayataguswa kwenye ubananaji huo wa matumizi, hivyo kasi ya miradi ya maendeleo itaendelea vile vile.
“Kama mlivyosikia, nilisema natoa ruzuku ya Shilingi bilioni 100 kufidia kwenye mafuta ili bei zishuke, na mwezi huu (Juni) bei zimeanza kushuka polepole,” Rais Samia aliwaambia wananchi kwenye ziara yake ya Bukoba jana.
“Tutaendelea kutoa hiyo ruzuku mpaka duniani kukae sawa. Tutaendelea kukata Shilingi bilioni 100 kila mwezi kwenye matumizi ya serikali tuweke ruzuku mpaka bei zikae sawa.”
Rais Samia amesema kuwa lengo la uamuzi huo ni kupunguza makali kwa wananchi yanayotokana na upandaji wa bei za mafuta kwenye soko la dunia.
Aliongeza kuwa kutokana na ruzuku hiyo ya Shilingi bilioni 100 kila mwezi, bei za mafuta nchini zitaendelea kushuka hadi zifikie hali ya zamani ya utulivu.
Uamuzi wa Rais Samia kuweka ruzuku kwenye mafuta umepokelewa kwa shangwe na watu kila kona ya nchi.
Jijini Dar es Salaam, madereva teksi, waendesha pikipiki na bodaboda wamempongeza Rais Samia kwa kuwajali wanyonge kwa kuweka ruzuku kwenye mafuta.
Umoja wa Wamiliki na Waendesha Pikipiki na Bajaji Wilaya
ya Tanga Mjini (UWAPIBATA) unampongeza Rais Samia kwa hatua madhubuti anazochukua
kuhakikisha kuwa ongezeko la bei ya mafuta kwenye soko
la dunia hazileti athari kubwa katika maisha ya wananchi na uchumi wa Tanzania kwa ujumla.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ruzuku ya Shilingi bilioni 100
ya Rais Samia imesaidia kupunguza beiya mafuta, ambapo kwa bandari ya Tanga, petroli imeshuka kwa shilingi 152 kwa lita na dizeli imeshuka kwa shilingi 476 kwa lita.
Nao waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda mkoani Kagera nao wamempongeza Rais Samia kwa kupunguza gharama za mafuta.
Pongezi za bodaboda hao zimewasilishwa na Umoja wa Bodaboda wilayani Bukoba (UBOBU) ikiwa ni siku moja kabla ya Rais Samia kufika mkoani Kagera kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani humo.
Mwenyekiti wa UBOBU, Mahamud Sued amesema ushushaji wa bei ya mafuta utalisaidia kundi kubwa la bodaboda kuweza kumudu gharama za maisha na kuepuka kujiingiza kwenye vitendo viovu.
“Ili kutambua ukubwa wa kundi hili kwa upande wa Manispaa ya Bukoba pekee kuna bodaboda 8,600 ndio maana tunaomba aendelee kutupunguzia gharama.
Ruzuku imetolewa kwa wakati muafaka na kutupa nahueni sisi ambao riziki zetu zinategemea sana bei ya mafuta.”