Rc gambo azindua vifurushi vipya vya bima ya afya nhif, awasilisha ombi la mkopo wa x-ray, mri

Mwenyekiti wa mfuko wa bima ya afya ya NHIF Anne Makinda akihutubia wananchi katika viwanja vya Mbauda Jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa vifurushi vipya vya bima
Wananchi wa Arusha wakipata burudani wakati wa uzinduzi wa vifurushi vipya vya bima ya afya ktika viwanja vya Mbauda Jijini Arusha
Wanufaika wapya wa Bima ya afya wakiwa wameshika kadi zao za kupatia huduma katika picha ya pamoja na Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo akimkabidhi mmoja wa wananchi wa Arusha kadi ya bima ya afya
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo akikabidhi wateja wapya wa huduma ya afya kupitia vifurushi vya jipimie

Na
Seif Mangwangi, Arusha
MKUU
wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, ameuomba uongozi wa mfuko wa bima ya afya
NHIF, kuangalia uwezekano wa kuupatia mkoa huo mkopo wa fedha kwa ajili ya
kununulia  mashine za X-Ray, CitiScan na MRI, kwa ajili ya kurahisisha vipimo
kwa wagonjwa mbalimbali wanaofika katika hospitali ya rufaa ya Mount Meru, kwa
ajili ya matibabu.
Gambo,
ametoa ombi hilo leo alipokuwa akizindua rasmi  vifurushi vipya vya mfuko
wa bima ya afya vilivyoboreshwa katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya
Mbauda jijini Arusha na kusema kuwa hiyo ni aibu kwa hospital ya rufaa ya Mount
Meru,kukosa mashine za kupimia magonjwa ya binadamu.
Amesema
Mkoa wa Arusha ni mkubwa na hospital ya rufaa ya Mount Meru ni kongwe lakini
imekuwa ikikosa mashine za kutibu magonjwa muhimu ambayo yamekuwa yakisumbua
watanzania wengi.
“Ndugu
Mwenyekiti wa bodi, pamoja na Mkurugenzi wako napenda kutumia nafasi hii
kuwasilisha ombi rasmi la kuomba mkopo wa kununulia mashine kama za X ray, MRI
na CitiScan na mimi mwenyewe nitakaa pamoja na viongozi wa hospitali kuona
namna ya kuwasilisha ombi hilo mezani kwako,”amesema.
Gambo,
amesema miongoni mwa faida zinazopatikana na mfuko wa bima ya afya ni pamoja na
kusaidia uboreshaji wa miundo mbinu ya Zahanati,Vituo vya afya, Hospitali na pia
kuhakikisha upatikanaji wa dawa  kulingana na mahitaji.
Pamoja
na kupatikana kwa wataalamu wa afya, kutokana na  upungufu uliopo
 maeneo ya vijijini kupitia mpango wa matumizi ya Vifurushi vya matibabu
hilo litatatuliwa.
Amesema
kupitia uzinduzi huo wananchi wanapata elimu kuhusu mfuko wa bima ya afya na Serikali
imeweka mkakati  kuhakikisha huduma za afya zinaboreka
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa mfuko huo wa bima ya afya,Anne
Makinda, amesema mfuko huo ulianzishwa mwaka 2001 ulikuwa ukilenga watumishi wa
serikali tu na watu binafsi walikuwa wakichangia kwa gharama kubwa ya Shilingi
Milioni 1.5 .
Amesema
watumishi wa serikali walikuwa ni kikundi cha watu wachache sana  na hivyo
kujikuta kundi kubwa la wananchi ambalo ni asilimia kati ya 80% hadi 90 %
 wakiachwa nje ya huduma za mfuko huo.
Makinda,
amesema kuwa hicho kilikuwa ni kikwazo hivyo kukafanyika maboresho na kuwezesha
kuanzishwa kwa huduma ya Vifurushi vilivyoboreshwa hivyo akawaomba wananchi
wawekeze ili waweze kupata huduma ya matibabu kupitia mfuko huo wa bima ya
afya.
Amesema
hadi kufikia mwaka huu mfuko huo umetoa mikopo ya shilingi ya bilioni 26 ambapo
vituo 293 vya afya nchini vimenufaika huku mkoa wa Arusha ukiwa umeshapatiwa mkopo
wa shilingi milioni 820 na kwamba malengo ya mfuko ni kuendelea kutoa  mikopo ya vifaa tiba na dawa lengo ikiwa ni
kuboresha huduma za afya.
Kwa
upande wake mkurugenzi mkuu wa mfuko wa bima ya afya Bernad Konga, amesema kuwa
tayari wameshafanya mazungumzo na Wapagazi wa mkoa wa Arusha ili nao wajiunge
kwenye mfuko huo kama yalivyo makundi mengine ya kijamii yakiwemo Bodaboda,
Mama lishe na Machinga.
Amesisitiza
kuwa mwananchi akiwa na Bima ana uhakika na maisha yake hivyo akahamasisha
wananchi kujiunga na mfuko huo wa bima ya afya ili waweze kupata huduma bora ya
afya ambazo kwa sasa gharama za matibabu ni kubwa bila bima hawawezi kuzimudu.