Na Seif Mangwangi, Arusha
WAKAZI wa Halmashauri za Mkoa wa Arusha wametakiwa kushirikiana na viongozi wa halmashauri zao kuwafichua wahalifu watakaoharibu miundo mbinu ya anuani za Makazi wakati na baada ya zoezi hilo kukamilika.
Wito huo umetolewa na mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongella wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo leo Jumamosi, Februari 12, 2022 katika zoezi lililokutanisha wakuu wa wilaya, wakurugenzi, wenyeviti wa Halmashauri , kamati za ulinzi na usalama na wataalam mbalimbali wa Halmashauri hizo.
Mongela amesema haiwezekani Serikali iweke miundombinu hiyo halafu itokee baadhi ya watu wanaihujumu kwa kuiondoa mahali ilipowekwa.
“Kuna baadhi ya watu wamekuwa kazi yao ni kuhujumu Serikali, wanatoa chuma za anuani za makazi na kwenda kuziuza hivyo ni vyema wakuu wa wilaya na viongozi wa halmashauri mkashirikiana na jamii kuwakamata ili wachukuliwe hatua na kuwa funzo kwa wengine,”alisema.
Amesema uwekaji wa anwani za makazi unamhusu kila mmoja kuanzia mwananchi pamoja na viongozi wa mkoa hivyo ni vyema zoezi hilo likasimamiwa ipasavyo katika utekelezaji wake.
“Napenda kuliweka sawa jambo hili kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi liwe shirikishi katika kuwahusisha viongozi wote wa ngazi zote kwa kufanya hivyo laweza kukamilika hata mwezi aprili 2022,” amesema Mongella.
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Pima amesema kwa upande wa halmashauri ya Jiji walianza uwekaji wa anwani tangu mwaka 2008 ambapo zilifanyika kwenye kata nane ikiwa nne ndizo zilizokamilika na sasa wanaendelea kuzikamilisha.
“Niwaombe wananchi wa jiji la Arusha pamoja na viongozi mbalimbali kushirikiana katika zoezi hili ikiwa maana ya alama hizi ni kwamba hatutakwenda posta badala yake tunaletewa barua nyumbani pia zitaondoa gharama za kufungua sanduku la posta,”amesema