Sanders hatimaye amuidhinisha biden kama mgombea urais ili kumkabili trump

Seneta
wa jimbo la Vermont la Marekani, Bernie Sanders, Jumatatu
alimuidhinisha aliyekuwa makamu wa rais Joe Biden kuwa mgombea wa urais
kwa chama cha Democratic.


Katika
mawasiliano kupitia njia ya video iliyowaunganisha wawili hao, Sanders
aliahidi kumsaidia Biden kushinda uchaguzi wa Novemba mwaka huu,
akimtaja Trump kuwa mtu hatari zaidi katika historia ya hivi karibuni ya
Marekani.

Sanders
na Biden walikuabliana kuunda tume maalum zitakazofanya kazi kwa pamoja
kuhusu maswala ya sera, jinsi ya kushughulikia maswala muhimu ya
mabadiliko ya hali ya hewa, afya na uhamiaji, miongoni mwa mengine.

Sanders
aliahidi kuleta Pamoja timu yake ya kampeni na kushirikiana na ya Biden
katika kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi Novemba mwaka huu.

“Tunakuhitaji
katika White House. Nitafanya kila niwezalo kuhakikisha kwamba hilo
linafanikiwa, Joe,” Sanders alimwambia Biden katika video iliyowekwa
kwenye wavuti wa Biden na kusambazwa kwa mitandao ya kijamii.

Seneta
huyo alimkosoa Rais Trump kwa jinsi amesimamia janga la maambukizi ya
virusi vya Corona, pamoja na kumtaja kuwa mbaguzi mkuu wa rangi miongoni
mwa mengine, akisisitiza kwamba anastahili kuondolewa madarakani.

Hatua
ya Sanders kumuunga mkono Biden ambaye anakuwa mshindani wake mkuu
katika kinyang’anyiro cha tiketi ya chama cha democratic, ni muhimu sana
wakati chama hicho kinatafuta kuunganisha wafuasi wake dhidi ya Rais
Trump katika uchaguzi ujao.

Biden
alimshukuru Sanders kwa kumuidhinisha, akisema anamhitaji sana sio
kushinda kiti cha urais, lakini hata katika kuongoza Marekani.

“Nadhani
hatua yako ya kuniidhinisha ina maana kubwa sana. Ina umuhimu mkubwa
sana kwangu. nadhani kuna watu watashangaa kwamba baadhi ya sera zetu
hazifanani lakini tunakubaliana katika mambo mengi sana. Nitakuhitaji
sana sio tu kushinda uchaguzi bali pia kuongoza taifa,” alisema Biden
katika mazungumzo yao.

Biden,
akimtaja Sanders kuwa rafiki, alisema ana matarajio makubwa sana
kufanya kazi na Sanders akiahidi kufanya kila awezalo kutimiza matarajio
yao.

Hii
ni mara ya pili kwa Bernie Sanders, kuwania tiketi ya chama cha
democratic katika uchaguzi wa urais bila mafanikio. Mwaka 2016,
alishindwa na Bi Hillary Clinton.

Credit-VOA