Serikali yamaliza mgogoro wa uendeshaji kinu cha nafaka arusha.

HATIMAYE mgogoro wa muda mrefu wa uendeshaji wa kinu cha kusagisha nafaka kilichopo Arusha kati ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko na Kampuni ya Monaban Trading and Farming ya jijini Arusha umemalizika baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuingilia kati.

Kufuatia kumalizika kwa mgogoro huo na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kukabidhiwa uendeshaji wa kinu hicho, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri Kilimo, Japhet Hasunga aisimamie Bodi hiyo na kuhakikisha inaendeleza kinu hicho ili kiwe na tija kwa wakulima na Taifa kwa ujumla.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumatano, Juni 12, 2019) wakati alipokutana na Waziri wa Kilimo pamoja na Viongozi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ofisini kwake Bungeni jijini Dodoma. Awali kinu hicho kilikuwa kinamilikiwa na Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC).

Amesema Waziri wa Kilimo ahakikishe kuwa kinu hicho kinasagisha nafaka kwa wingi kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi na ziada ya unga utakaozalishwa kuuzwa nje ya nchi ili nchi iweze kupata faida zaidi kwa kuuza unga utaotokana na kinu hicho.

Uamuzi wa kukabidhi kinu hicho cha kusagisha nafaka kilichokuwa kikiendeshwa na Kampuni ya Monaban Trading and Farmning kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ulitolewa na Baraza la Mawaziri katika kikao kilichofanyika mwaka 2008.

Mgogoro huo wa uendeshaji wa kinu hicho ulitokea baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Monaban Trading and Farming, Dkt. Philemon Mollel kutoelewana na uongozi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kuhusu uendeshaji wa kinu hicho hali iliyosababisha Waziri Mkuu kuingilia kati.

Waziri Mkuu amesema bodi hiyo inamiliki vinu vinne vilivyopo Arusha, Dodoma, Iringa na Mwanza. Kinu cha Arusha pekee ndicho kilichokuwa na migogoro ya mara kwa mara ambayo haikuwa na utatuzi kwa muda mrefu licha ya jitihada za Serikali kutatua mgogoro huo.

“Viongozi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko waliwahi kufungiwa milango na mwekezaji aliyesaini mikataba ambayo haieleweki na akawa anaonekana anataka kukirasimisha Kinu cha Arusha kiwe mali yake na ndipo tukalazimika kuunda Timu ya uchunguzi ili kubaini uhalali wake na kuchukua hatua stahiki”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *