Shinyanga kuhakikisha hakuna mwanafunzi atakayekosa nafasi kidato cha kwanza

 Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Serikali ya Mkoa wa Shinyanga imesema itahakikisha kila mwanafunzi aliyefaulu kuingia  kidato cha kwanza Mwaka huu 2022, anajiunga kuendelea na masomo na kwamba haitakubali kuona mwanafunzi anashindwa kuendelea kwa sababu zisizo za msingi.

Hayo yamesemwa leo na katibu tawala wa Mkoa wa Shinyanga Zuwena Omary ambapo ameeleza kuwa ujenzi wa vyumba vya madarasa umekamilika na kwamba mazingira ni rafiki kwa wanafunzi na walimu kufundishia hivyo amesema hakuna sababu ya wanafunzi kukaa nyumbani.

Katibu Zuwena Omary amewataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao kwa kuwapatia watoto mahitaji yao muhimu ikiwemo yunifomu za shule na mahitaji mengine ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa na serikali katika kutengeneza Taifa bora.

“Wazazi wote wanao wajibu kama serikali imetimiza wajibu basi na wazazi wanapaswa kutimiza wajibu wao kisheria lakini pia kijamii kwa sababu malezi ya mtoto niya mzazi kwahiyo kuwapatia wanafunzi mahitaji yao muhimu kwa ajili ya kujiunga na kidato cha kwanza ni wajibu wao”.

“Uwepo wa madarasa ambapo wanafunzi watakaa kwa nafasi walimu wataweza kuwasiliana na wanafunzi bila msongamano kwenye darasa moja italeta tija kwahiyo madarajio ni kwamba hali ya ufaulu itapanda”.

Aidha Zuwena amewataka wanafunzi wote wanaoendelea na masomo na wale wanaotarajia kuanza masomo yao Mwaka huu kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kusoma kwa bidii na kwamba kama kuna changamoto wazifikishe sehemu husika ili ziweze kushughulikiwa.

“Matarajio ni kwamba wanafunzi wote waliochaguliwa wanayonafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza kwahiyo nitoe wito kwa wanafunzi wote ambao wamechaguliwa na wale wanaoendelea kwamba elimu ni kwa faida yao kwanza kwa kuondoa ujinga na kujipanga kwa ajili ya maisha yao ya badae iwapo kuna mwanafunzi atataka kukatishwa ndoto zake za kutaka kujiunga shuleni   wakati mwingine wanaweza kusababisha wazazi au mazingira anayoisha basi kwa haraka sana atoe taarifa kwenye ofisi ya serikali aliyokaribu nayo na sisi tutasimamia kuhakikisha tunafuatilia wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wanajiunga wote na wale ambao tutakuta wana changamoto tutachukua hatua kama changamoto ya mzazi tutakabiliana na mazazi husika”.

Serikali ilitoa fedha kwa kila mkoa kote nchini kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kama mpango maalumu wa kukabiliana na maambukizi ya UVIKO-19 kwa maendeleo ya Taifa.