Na Mapuli Misalaba,Shinyanga
Wakazi wa kata ya Kambarage Manispaa ya Shinyanga wameiomba serikali kuona namna bora ya kuongeza taasisi za elimu hasa vyuo vikuu ikiwa ni pamoja na kuwekeza viwanda mbalimbali ikiwemo vinavyozalisha vifaa vya ujenzi.
Wananchi hao wamepongeza mpango wa serikali wa kuboresha miundombinu katika sekta za afya na elimu ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa,ambapo wameiomba serikali kuweka msukumo ili kuhakikisha mkoa wa Shinyanga unawekeza katika viwanda hasa vinavyozalisha vifaa vya ujenzi hali itakayochangia kuwa na mapinduzi ya kiuchumi kutokana na fursa mbalimbali zitakazojitokeza
Wametoa kauli hiyo wakati wakishiriki katika shughuli ya kuchimba na kufukia msingi ikiwa ni hatua ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya sekondari Mwasele iliyopo kata ya Kambarage ambapo wananchi wamejitolea nguvu zao kuunga mkono jitihada za serikali
Wakazi wa Manispaa ya Shinyanga wameendelea kujitokeza kushiriki katika shughuli za kuchimba msingi katika ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuunga mkono mpango wa serikali ambayo imetoa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika shule mbalimbali za sekondari