Shughuli za kibinadamu zinavyohatarisha bonde oevu la kilombero

 


Na Mwandishi wetu

BONDE la Kilombero lilitengwa kuwa Pori Tengefu kwa Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Sura ya 302 ya mwaka 1952 (Fauna Conservation Ordinance CAP 302 of 1952 GN.No.107) likiwa na ukubwa wa km za mraba 6,500. Aidha Serikali ilitenga bonde hilo kuwa Pori Tengefu tena kwa Tangazo la Serikali Namba 459 la mwaka 1997.

Sababu kubwa ya Serikali kuweka mikakati ya kulilinda ni kutokana tafiti nyingi za ndani na nje ya nchi kubaini kuwa Bonde la Kilombero ni umuhimu kitaifa na kimataifa. Kama hiyo haitoshi, bonde likaorodheshwe kidunia kuwa eneo la Ramsar (eneo linalopaswa kutunzwa na kulindwa tarehe 24/04/2002 na kupewa namba 1173 (W1 ItZ03). Eneo la Ramsar la Kilombero lina ukubwa wa Kilometa za mraba 7,967.35 sawa na Hekta 795,735 na kuwa eneo la 3 lenye umuhimu wa kimataifa Tanzania.

Umuhimu wa bonde hili umekuwa ukisababisha Serikali kuja na mikakati mbalimbali ya kulilinda, mfano mwaka 2006 Makamu wa Rais aliagiza kuondoa wavamizi wa bonde la Kilombero, hii ilifuatia uhaba wa umeme uliotokana na ukosefu wa maji katika mabwawa ya Mtera na Kidatu. Ukosefu huu ulitokana na mifugo na kilimo kisichoendelevu kwenye vyanzo vya maji vinavyolisha mabwawa hayo hasa bonde la Kilombero.

Morsadi Simbamkuki (81) ni mkazi wa Mtaa wa Mahakama, Ifakara anasema licha ya kuonekana umuhimu huo, bonde hilo kwa sasa limeendelea kuvamiwa na wafugaji hivyo kuhatarisha uwepo wake kwani idadi ya mifugo ni kubwa mno.

Morsadi anaungana na wananchi wengi wanaoishi kuzunguka bonde hilo ambao wanasema uko umuhimu wa kuongeza nguvu kulinda bonde hilo kwani linapoharibiwa, wa kuumia sio wakazi wa Kilombero bali Taifa na ulimwengu kwa ujumla. Kwa mfano maji yanayotarajiwa kwa ajili ya mradi wa Umeme wa Nyerere kwa asilimia 62.5 unategemea maji ya Bonde la Kilombero.

 

Kwanini tufikirie kuhifadhi misitu na vyanzo vya maji?

Mwl J.K Nyerere akiwa Mwanza tarehe 25/03/1986 kwenye mkutano alinukuliwa akisema  “Tutakuwa ni wezi kama tunahujumu misitu na vyanzo vya maji kwa kuwa ni sehemu ya ardhi na ardhi siyo mali yetu ni mali ya wajukuu na vitukuu.Wanapashwa kutupiga viboko wakiukosa utajiri huu”.

Kutokana na umuhimu wa Bonde hili kumekuwa na miradi mbalimbali ikiwamo ule ulioitwa
Mradi wa KILORWEMP yaani kifupi cha “Kilombero and Lower Rufiji Wetlands Ecosystems Management Project”

Mradi huu ulianza kutekelezwa mwaka 2012 baada ya mradi wa awali wa kusaidia kuhifadhi bonde kumalizika mwaka 2011 uliojulikana kwa jina la Kilombero Valley Ramsar Site Project (KVRS)

Chimbuko la mradi huu ulikuwa ni Msaada kutoka Ubelgiji kupitia BTC na mradi mwingine wa kuendeleza yaliyoanzishwa na mpango wa “Sustainable wetlands management (SWM)” wa Idara ya Wanyamapori uliofadhiriwa na 

Shirika la Maendeleo la Denmkark (DANIDA).

Lengo kuu la mradi lilikuwa ni kuleta Ufanisi katika kutunza ikolojia ya aridhi oevu ya bonde la Kilombero na mto Rufiji ili kuhifadhi bianua na kuwezesha jamii kunufaika kiuchumi kutokana na maji na maliasili. Lengo jingine lilikuwa ni kuongeza uwezo katika kusimamia sera na miongozo ya ikolojia ya ardhi oevu katika bonde la Kilombero na mto Rufiji kwa lengo la kuwezesha ugatuzi katika usimamizi wa maliasili ili kuinua hali ya maisha ya jamii.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja anasema Bonde la Pori tengefu la Mto Kilombero ni muhimu Kitaifa na Kimataifa kutokana na uhifadhi wa bionuwai zilizo adimu Duniani kama vile mnyama aina ya sheshe.

Naibu waziri anakwenda mbali zaidi kusema kuwa Bonde la Pori Tengefu la Kilombero ni sehemu ya ardhioevu linalochangia asilimia 62.5 ya maji yote ya mto Rufiji hivyo kuwa chanzo muhimu cha maji kwa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere. Kwamba, Bonde hilo lina umuhimu kitaifa na Kimataifa kutokana na uhifadhi wa bionuwai zilizo adimu Duniani kama vile mnyama aina ya sheshe ambao hawapatikani maeneo mengine.

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka Biswalo Mganga akiwa Ifakara akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Kilombero aliagiza wananchi wanaofanya shughuli za kilimo katika maeneo ya hifadhi kusitisha shughuli hizo  na kwenda kutafuta sehemu nyingine za kuendeshea shughuli zao ili kulinda mazingira.

Mganga anasema wakati wote maslahi ya Taifa yanatangulia maslahi binafsi hivyo ulinzi wa hifadhi ni jambo. Anasema bonde la Kilombero ni eneo linalotegemewa sana katika mradi wa Umeme wa Mwalimu Nyerere unaojengwa Rufiji Pwani hivyo uharibifu wa maliasili katika bonde hilo haukubaliki hata kidogo.

Kwa mujibu wa Mganga wapo watumishi wa Serikali wanaenda kulima na kufuga katika maeneo ya Bonde la mto Kilombero hivyo aliwataka waache kufanya hivyo kwa kuwa wanaharibu mazingira.

Serikali imewekeza fedha nyingi katika mradi wa Umeme wa Mwalimu Nyerere na Bwawa hilo kwa kiasi kikubwa linategemea maji kutoka Kilombero hivyo uharibifu ukitokea halafu maji yakikosekana  Taifa litakuwa limepoteza fedha nyingi, fedha za Taifa zitakuwa zimepotea.

Muendelezo wa shughuli za kilimo kwenye maeneo hayo kutaifanya nchi yetu kuendelea kuagiza umeme kutoka nje ya nchi, viwanda vyetu vitaendelea kukosa umeme wa uhakika.

Licha ya kauli hiyo nzito uharibifu wa mazingira bado unaendelea katika bonde hilo huku  mifugo ikiendelea kuonekana pamoja na shughuli nyinginezo kuendelea kama kawaida, jambo linalosababisha baadhi ya wananchi kuuliza ni kwanini hakuna hatua thabiti zinazochukuliwa kuzuia kabisa vitendo hivyo.

Uchunguzi uliofanywa katika maeneo mbalimbali ya halmashauri na wilaya za Mlimba, Malinyi, Kilombero, Ulanga na Ifakara zinaonyesha kuwa shughuli za kibinadamu zinaendelea sana katika bonde la Kilombero licha ya ukweli kwamba maeneo hayo yanazuiwa na sera za nchi na zile za kimataifa kutumika kwa shughuli hizo za kibinadamu.

Katika bonde la Kilombero linalounganisha halmashauri na wilaya hizo ni kawaida kuona utitiri wa mifugo kwenye bonde hilo ikila hadi maeneo ambayo wakati wa masika hutumika kama mazalia ya samaki, kitendo ambacho kinatia hofu juu ya hatma ya samaki.

Baadhi ya wananchi wanaomba Serikali kuchukua hatua ikiwamo kuhakikisha mifugo inaondolewa yote kwani mifugo ndiyo inayoonekana kuharibu kwa kiasi kikubwa mazingira. Maeneo hayo kihistoria yamekuwa sio ya wafugaji, isipokuwa wakiingilia hivi karibuni, maeneo hayo yanajulikana kama eneo la wakulima ambao wamekuwa wakilima mbali na mito, tofauti na wafugaji ambao huingiza mifugo kwenye bonde hivyo kuharibu vyanzo vya maji.