Siyo kweli rais samia kaamuru mbowe aachiwe huru

Na Frankius Cleophace.

Kutokana na kukua kwa teknolojia, vyombo vya habari vimekuwa vikihabarisha habari zao kwa kutumia mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, Twitter, Instagram. Youtube na WhatsAp.

Mitandao ya kijamii imekuwa njia rahisi na ya haraka ya kufikisha habari kwa watu hasa wanaotumia simu za mkononi na kompyuta.

Hata hivyo, baadhi ya wamiliki wa chaneli za YouTube wamekuwa wakitumia njia zisizo sahihi kupata watazamaji wa video zao kwa kutunga habari za uzushi na zinazopotosha watu. 

Moja ya mbinu inayotumika ni kuandika vichwa vya habari ambavyo ni tofauti na maudhui ya habari husika. Wakati mwingi habari hizo huwahusisha watu maarufu na viongozi wa Serikali.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na habari katika mtandao wa YouTube inayodai Rais Samia Suluhu Hassan ameamuru Mwenyekiti wa Chadema anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na ugaidi aachiwe huru, jambo ambalo siyo sahihi.

Ukweli uko wapi?

Habari hiyo ambayo bado inatazwa na watu katika mtandao wa YouTube inapotosha kwa sababu Rais Samia hajawahi kutoa tamko la namna hiyo mahali popote.

Kesi hiyo ya Mbowe na wenzake watatu iko mahakani na Rais hawezi kuingilia uhuru wa mahakama kufanya maamuzi. 

Hata alipohojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) Agosti 9, 2021, Rais Samia alisema kesi ya Mbowe iachiwe mahakama ndiyo itatenda haki. 

Pia kwa kutumia zana mbalimbali za kidijitali ikiwemo InViD, Google Image kubaini habari hiyo ya Rais kuamuru Mbowe aachiwe kama imeripotiwa na vyombo vingine vya habari, hatukuweza kufanikiwa kuipata.

Waandishi wa habari wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia taaluma yao ili kuepuka kuwa sehemu ya kusambaza habari za uzushi ambazo zinaweza kuleta madhara kwenye jamii.