Smart community na wadau wake watoa tabasamu kwa wazee meru.

 

Na Mwandishi Wetu,

Arusha.

KATIKA kuelekea sikukuu ya Pasaka Shirika la Smart Community on Legal Protection la Jijini Arusha kwa kushirikiana na wadau wake wamewatembelea na kuwapa msaada wazee wa kituo cha Meru Elderly Initiatives kilichopo Kata ya Kikatiti Wilaya ya Arumeru Jijini hapa.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo Mkurugenzi wa Shirika hilo Wakili Mary Mwita amesema kusaidia wenye uhitaji ni tendo la kumpendeza Mwenyezi Mungu kwa kuwa ametuasa kupendana.

Aidha Wakili Mwita amewapongeza watoa huduma wote katika kituo hicho kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kulea wazee ambao wapo kituo hapo kwa changamoto tofauti.

“Kwa niaba ya wanachama wa Smart Community, wadau na marafiki wote naomba niwapongeze watoa huduma wote wa kituo hiki kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kulea wazee hawa, muendelee na moyo huo wa upendo na Mwenyezi Mungu awabariki, sisi kuja hapa na kutoa msaada huu haimaanishi tuna pesa nyingi bali ni kutokana na upendo tulionao kwa wazee hawa” Alisema

Wakili Mwita alitaja vitu walivyopeleka kuwa ni pamoja na nguo, viatu, mchele, sukari, sabuni, mafuta ya kupikia, dawa za meno, mafuta kupakaa, pamoja na Juice.

Kwa upande wake Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Kanda ya Kaskazini Vonness Koka ameishauri jamii kuendelea kuwasaida wazee na ikiwezekana vituo vya kuwalea viongezwe kwa kuwa wazee wenye mahitaji ni wengi.

“Napata faraja Sana kuona jamii inaona umuhimu wa kuwatunza wazee wetu, hatua hii inatukumbusha kuwa na sisi ni wazee watarajiwa, huenda na sisi tukaja kuhitaji msaada kama wao, kwa hiyo naishauri jamii isichoke kuwasaida wazee wetu na hata kama Kuna uwezekano vituo vingi vianzishwe Ili kupunguza changamoto zinazowakabili” alisema Koka.

Naye Afisa Ustawi wa Jamii wa kituo hicho Remigius Bonajose alisema kituo hicho kina zaidi ya miaka ishirini na hadi sasa kinahudumia wazee 255 kutoka Kata tano na vijiji nane vya wilaya ya Arumeru ambao wapo nje ya kituo hicho huku wazee Saba wakilelewa ndani ya kituo.

“Wazee wengi wapo nje ya kituo kwa kuwa kituo kina uwezo wa kupokea wazee 24 tu, ambapo changamoto kubwa ipo kwa wale wazee wa nje kwa kuwa msaada tunaopeleka haukidhi mahitaji kwa kuwa wanaishi kwenye familia kubwa” alisema Bonajose.

Bonajose amesema kituo hicho kipo chini ya kanisa la International Evangelism na kinafadhiliwa na Dorcas Aid na kinapokea wazee kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Wakishukuru mara baada ya kupokea msaada huo Fanuel Summary na Ndewaramisa Lazaro wamesema msaada huo umekuja wakati muafaka kwa kuzingatia kuwa kesho ni sikukuu ya Pasaka hivyo na wao watasherehekea kwa furaha huku wakiwaomba wasamaria wema waendelee kuwatembelea kituoni hapo mara kwa mara hata kwa ajili ya kuwapa salamu tu.