Sophia mjema akabidhiwa rasmi ofisi ya mkuu wa mkoa wa shinyanga

 

Na Mapuli Misalaba,  Shinyanga

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema leo amepokelewa na kukabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa mkuu wa mkoa huo Dkt Philemon Sengati.

Hafla hiyo ya makabidhiano imefanyika leo Oktoba 12, mwaka huu 2021 mjini Shinyanga katika ukumbi wa mkuu wa mkoa na kuhudhuriwa na wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa Halmashauri, Wenyeviti wa Halmashauri, viongozi wa chama, viongozi wa dini, viongozi mbalimbali na kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Shinyanga

Akizungumza baada ya kukabidhiwa rasmi mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema amewataka viongozi wa serikali hasa wakuu wa idara kuwajibika kwa kutimiza wajibu wao huku wakisikiliza  na kutatua changamoto za wananchi 

“Kila mmoja katika nafasi yake anajua anatakiwa kufanya nini sitotegemea kuona jambo liko kwenye kata au mtaa mkuu wa mkoa au mkuu wa wilaya ndiye anakuja kulimaliza wakati kunamtendaji hatutakubali kila mtu katika eneo lake apange siku maalum za kuonana na wananchi wake tumechagua kuwatumikia wananchi ni lazima tuwasikilize kama kesi ndogo zinawafikia viongozi wa juu maana yake huko chini hamuwasikilizi  kama mnawasikiliza basi hamuwajibu vizuri”

Mjema amesema viongozi wasiwe chanzo cha mgogoro huku akisisitiza  viongozi kuwa wa mfano wa kuigwa na jamii ambapo amesema hatokubali  kuona ofisi zimefungwa wakati wananchi wanataka huduma

“Nataka viongozi mfanye kazi siku zote siku ya kupumzika ni siku ambayo utakapo kuwa kwenye likizo yako lakini siku za ibada ukitoka kwenye ibada hakikisha kazi inaendelea sitegemei kuona ofisi zimefungwa hasa watendaji wananchi watataka hudumu mtendaji hayupo ofisi ziwe wazi masaa 24 ili wananchi waweze kupata huduma”

Mkuu wa mkoa huyo amesema kila mkuu wa idara katika mkoa wa Shinyanga atapatiwa ilani ya chama cha mapinduzi ili kusiwepo na visingizio kwenye  wajibu na majukumu ya kufanya

Mjema amesema viongozi wasimamie vizuri fedha za serikali zitumike kwa matumizi yaliyoelekezwa  zisitumike hovyo 

“Fedha zilizotolewa na serikali zikija zisimamiwe kwa lile lililokusudiwa na sivinginevyo na mimi nitakuwa mkali sana kwa Manispaa ya yoyote itakayo kwenda kinyume na hapo”

Amekemea suala la mimba na ndoa za utotoni pamoja na imani za kishirikina ambapo amesema ataendelea kushirikiana na viongozi wa dini pamoja na wazee wa mila katika kuondoa changamoto hizo

“Lazima tukasimamie mimba za utotoni  hapa ni nyingi mno na wale wanao kamatwa wazazi wasilalamike kama mtoto akipatikana anaujauzito  apatikane aliyempa ujauzito na afunguliwe mashtaka kama mzazi akiingilia kusema watakubaliana na naye akamatwa nataka mimba za utotoni ziishe Shinyanga viongozi wa dini na wazee wa kimila tutashirikiana nao”

Pia mkuu wa mkoa Sophia Mjema amewaomba viongozi na wananchi wa mkoa wa Shinyanga  kuendelea kushirikiana huku akisisitiza kila mtu awajibike katika nafasi yake 

Kwa upande wake Dkt. Sengati amewashukuru wananchi wa mkoa wa Shinyanga kwa ushirikiano ambapo amesema wananchi waendelee na kushirikana na viongozi hivyo hivyo ili kujenga  umoja, upendo na kuendelee kudumisha amani ya Tanzania 

Sophia Mjema ambaye awali akiuwa ni mkuu wa wilaya ya Arusha, anakuwa mkuu mpya wa mkoa wa Shinyanga kufuatia hatua ya rais Samia Suluhu Hassan kutengua uteuzi wa aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt.Philemon Sengati kutokana na sababu ambazo hazijawekwa bayana.