Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga imesema kuwa inaendelea kufuatilia fedha zote za miradi ya maendeleo zilizotumika na zinazotarajiwa kutumika katika utekelezaji wa miradi hiyo ikiwemo Elimu na Afya.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Hussen Mussa amesema katika kipindi cha robo ya pili ya Mwaka wa fedha 2021/2022 TAKUKURU ilijikita katika kuzuia vitendo vya rushwa kwenye miradi 62 ya maendeleo inayotekelezwa mkoani humo.
“TAKUKURU Shinyanga ilifuatilia miradi 62 yenye thamani ya shilingi 4,127,494,475/= kati ya miradi hiyo 62 miradi 60 ni miradi ya ujenzi wa madarasa yenye thamani shilingi 4,085,996,434/= inayotekelezwa katika halmashauri zote sita za mkoa wa Shinyanga. Miradi miwili ni ya rasilimali kilimo yenye thamani ya shilingi 41,498,041/= inayotelekezwa katika kata za Mwamalili na Pandagichiza wilayani Shinyanga”,ameeleza Mussa.
Bwana Hussein ameongeza kuwa TAKUKURU Mkoa wa shinyanga ilifanya ufuatiliaji ili kuhakikisha fedha zilizotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo zinatumika ipasavyo na kuhakikisha hakuna ubadhirifu wala ufujaji wa fedha hizo.
“TAKUKURU Shinyanga ilifanya ufuatiliaji huo ili kuhakikisha kuwa fedha zilizotolewa kwa ajili ya miradi hiyo zinatumika ipasavyo na miradi inakuwa na thamani halisi ikilinganishwa na fedha iliyotolewa. Lengo jingine ni kuhakikisha kuwa hakuna ubadhirifu wala ufujaji wa fedha”,amesema.
“Mapungufu yaliyobainika katika ukaguzi wa miradi hii ambavyo yangeweza kusababisha mianya ya rushwa yamefanyiwa kazi kwa kufanya vikao na wadau ambao ni wasimamizi na watekelezaji wa miradi husika pamoja kutoa elimu kwa lengo la kuondoa mianya ya rushwa”,ameongeza.
Katika hatua nyingine Bwana Hussen ameongeza kuwa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga imepokea malalamiko 42 ambapo taarifa zilizohusu rushwa ni 20 na zisizohusu rushwa ni 22 na kuzitaja baadhi ya idara zilizolalamikiwa kuwa ni Ardhi, Elimu pamoja na serikali za mitaa.
Aidha amesema amesema kuwa mkakati mkubwa katika kipindi hiki ni kuendelea kutoa elimu hasa kwa vijana wa Skauti ili waweze kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa pamoja na kushiriki katika kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na kushiriki katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.
“Mkakati mkubwa kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2022 ni kuendelea kuto elimu kwa vijana wa Skauti ili waweze kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa na kuwajenga katika misingi ya kuwa waadilifu, wazalendo na wawajibikaji kwao na taifa lao. Pia washiriki kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na kushiriki katika kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao”,amesema.