Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga imepokea malalamiko 46 ambapo 27 kati yake yanahusisha taarifa za rushwa.
Katika taarifa yake ya utekelezaji wa taasisi hiyo katika kipindi cha robo ya kwanza ya Mwaka wa fedha 2021/2022, aliyoitoa leo kwa vyombo vya habari Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Mzee Mussa amesema ameeleza kuwa taarifa 20 uchunguzi wake unaendelea na kwamba malalamiko 7 uchunguzi wake umefungwa kutokana na kukosa ushahidi.
“Tumepokea malalamiko 46 taarifa zinazohuzu rushwa zilikuwa 27 kati ya hizo 20 uchunguzi wake unaendelea malalamiko 7 uchunguzi wake umefungwa kwa kukosa ushahidi taarifa zilizohusu rushwa zilikuwa 19 kati ya hizo malalamiko 3 yalihamishwa idara nyingine na malalamiko 16 watoa taarifa wake walishauriwa”.
Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga amesema kutokana na taarifa za malalamiko yaliyopokelewa na taasisi hiyo yanahusisha idara mbalimbali zikiwemo za serikali za mitaa,huku kesi 21 zikiendelea mahakamani.
“Idara zilizolalamikiwa ni serikali za mitaa (15), Elimu (6), Ardhi (4), Madini (4), Ujenzi (3), Afya (2), Siasa (2), Fedha (2), Biashara (2), Mahakama (2), Kazi (2), Maliasili (1), Barabara (1) kesi zinazoendelea mahakamani ni 21 kata ya hizo kesi mpya ni tatu (3)”.
Katika taarifa yake ya utekelezaji katika kipindi cha robo ya kwanza ya Mwaka wa fedha 2021/2022 iliyoanzia Julai –Septemba Mwaka huu amesema taasisi hiyo imekuwa na utaratibu wa kuwafuata wananchi kwenye maeneo yao ili kuwapa elimu sahihi kuhusu madhara ya rushwa lakini pia kusikiliza kero zao.
“Ofisi ya TAKUKURU mkoa wa Shinyanga imeweka utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi siku moja kila mwezi kwa kuwafuata wananchi katika maeneo yao ambapo kipindi cha Julai, 2021 TAKUKURU mkoa wa Shinyanga ilitembelea na kusikiliza kero katika kata tatu (3) ambazo ni Kambarage, Kishapu na Nyamilangano”.
Mkuu wa TAKUKURU amesema taasisi hiyo imeendelea na jukumu lake la kuelimisha umma huku ikitoa kipaumbele kuhamasisha wananchi ili kushirikiana na takukuru katika mapambano dhidi ya rushwa.
Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga ameeleza kuwa katika kipindi cha Julai-septemba taasisi hiyo ilijikita zaidi kwenye uzuiaji wa rushwa kwenye miradi inayotekelezwa na fedha za Serikali pamoja na ufadhili wa wadau ikiwa imelenga kudhibiti matumizi mabaya ya rasilimali fedha
“TAKUKURU mkoa wa Shinyanga ilijitahidi kuzuia rushwa kwenye miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoa mzima wa Shinyanga uzuiaji huo unafanyika ili kuhakikisha kwamba fedha zilizotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo zinatumika ipasavyo na kuhakikisha kuwa hakuna ubadhirifu wala uvunjaji wa fedha hizo”.
Amesema kuanzishwa kwa mfumo wa TAKUKURU tembezi Mkoani Shinyanga imechangia kupungua kwa mianya ya rushwa kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali.
Amesema elimu hiyo inayotolewa kwa jamii kupitia mfumo wa huduma tembezi imesaidia wananchi kuhamasika na kuwa sehemu ya wasimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa, hali ambayo imechangia kupunguza mianya ya rushwa.