Takukuru yaagizwa kuchunguza utitiri matapeli wa ardhi kata pangani, kibaha *viongozi wa kisiasa, serikali watajwa kuhusika, wadaiwa kujificha migongoni mwa watu wasionekane *shule hazina madawati ya kutosha watoto wanakaa chini, huku matapeli yakivuna mamilioni kwa kuuza ardhi ikiwamo ya mitamba ambayo ni mali ya serikali *mawaziri wa ardhi na mifugo waombwa kuingilia kati

Na Dismas Lyassa, Kibaha Mjini

“NAAGIZA TAKUKURU fuatilieni suala la migogoro ya ardhi,” ni kauli ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya Kibaha Mjini, Maulid Bundala alipofanya ziara kutembelea Mtaa wa Vikawe kwa lengo la kuzungumza na viongozi na wananchi kuhusu migogoro ya ardhi inayoendelea katika eneo hilo.

Ziara hiyo ambayo ilishirikisha wajumbe wa Kamati ya siasa CCM Wilaya Kibaha Mjini ilifanyika kufuatilia hivi karibuni wananchi kufunga ofisi ya Serikali ya Mtaa kutokana na mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na viongozi wao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wameshauri vyombo vya dola kufanya uchunguzi kwa kuwatambua wanaoendeleza utapeli wa viwanja katika Kata Pangani na kuchukua hatua kwani baadhi yao wanadaiwa kuwa ni viongozi.

“Ukweli ndugu mwandishi, migogoro ya ardhi ina athari kubwa sana kwa jamii, unakuta mtu anajenga nyumba halafu anaambiwa hiki kiwanja sio chako… mambo kama haya ni ya kawaida sana katika Kata hii ya Pangani, bahati mbaya sana wanaofanya utapeli wanafahamika, inadaiwa hawachukuliwi hatua kwa sababu ni mtandao unaonufaisha hadi baadhi ya wakubwa juu, wanatumia rushwa na wengine wanakesha kwa waganga kutafuta dawa za kutapeli watu ardhi,” alisema mkazi mmoja wa Vikawe Shuleni ambaye hakupenda jina lake litajwe.

Kwa upande wake Bi. Zamda Komba, ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa CCM Wilaya Kibaha Mjini alisema Pangani ndio kata inayoongoza kwa migogoro ya ardhi katika wilaya nzima ya Kibaha Mjini, sifa ambayo sio nzuri, hivyo akashauri jitihada zifanywe kuondokana na sifa hiyo mbaya.

Hata hivyo baadhi ya wananchi wana hofu kama sifa hii inaweza kuondoka Kata Pangani wakidai vinara wakuu wa utapeli wa ardhi ni baadhi ya viongozi, ambao wengine wanahusika moja kwa moja kuuza hadi ardhi ya Mitamba ambalo ni mali ya Serikali, ilikuwa inatumika kulishia mifugo ambalo sasa halitumiki. Baadhi ya viongozi wanadaiwa kujikatia ardhi watakavyo katika ardhi hiyo ya Serikali wakitumia majina  jamaa zao. Aidha baadhi ya viongozi ambao ndio walipaswa kuwa kimbilio la wananchi wasitapeliwe tayari wana kesi walizofunguliwa na wananchi wakiwatuhumu kuchukua ardhi zao.

“Kata Pangani ina changamoto nyingi, kwa mfano Shule nyingi zilizoko ikiwamo Shule ya Msingi na Sekondari Kidimu, hazina madawati ya kutosha, watoto wanakaa chini, huku matapeli yakivuna mamilioni kwa kuuza ardhi ikiwamo ya Mitamba ambayo ni mali ya Serikali… ni bora wangeelekeza fedha katika maendeleo,” anasema mkazi mwingine wa Vikawe Shule na kushauri mawaziri wa Mifugo na yule wa Ardhi kuja Kata Pangani ili kuchukua hatua dhidi ya eneo la Mitamba na kupewa orodha ya matapeli wanaoumiza wananchi katika Mitaa mbalimbali ya Kata Pangani ili hatua ziweze kuchukuliwa.

Mwisho