Tanapa yatoa tozo mpya kuingia hifadhini, yashusha bei kuvutia watalii zaidi

NA GRACE MACHA, ARUSHA
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa nchini, (TANAPA), imefanya mabadiliko ya
tozo kwa kupunguza viwango kwa baadhi ya bidhaa za utalii huku
wakianza tozo mpya ya kuingia hifadhini zaidi ya mara moja, (multiple
entry).
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Mawasiliano wa shirika hilo, Pascal
Shelutete amewaeleza waandishi wa habari ofisini kwake leo julai 30,
kuwa mabadiliko hayo ya  tozo yanaanza kutumika rasmi Agosti mosi
mwaka huu mpaka juni 30, mwakani.
 Amesema tozo ya kuingia hifadhini zaidi ya mara moja itakuwa ya
aina mbili tofauti ambapo kwa wageni wanaolala ndani ya hifadhi
watapewa kibali cha saa 24  huku wale wanaolala nje ya hifadhi
wakipewa kibali cha saa 12.
“Tofauti iliyopo kati ya vibali hivyo viwili ni kuwa kibali cha saa 12
kitaisha inapofika saa 12 jioni bila kujali kilikatwa muda gani wa
siku husika. Ndani ya saa 12 ya kibali mgeni anaweza kutoka na kurudi
hifadhini bila kulipia tozo ya ziada,” anasisitiza.
Amesema kuwa kibali za saa 24 kitadumu kwa kipindi cha saa 24 tangu
kilipotolewa na ndani ya muda huo na mgeni anaweza kutoka na kurudi
hifadhini bila kulipa tozo ya ziada.
“Uamuzi huu wa serikali unalenga kuinua utalii wa kiutamaduni kwenye
maeneo ya wananchi yaliyo nje ya hifadhi za Taifa ambapo wageni hasa
watalii walishindwa kuyatembelea kwa kuhofia kulipia tozo mara mbili,”
amesema Shelutete na kuongeza.
“Uamuzi huu unatarajiwa kuinua utalii wa kiutamaduni kwenye maeneo
hayo pamoja na kuongeza kipato cha wananchi katika maeneo hayo na
hivyo kufaidika na uwepo wa hifadhi katika maeneo wanayoishi,”.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi huyo wa Mawasiliano amesema katika
jitihada za kuvutia watalii kutembelea hifadhi, serikali imepunguza
tozo kwa utalii wa kutembea (Canopy walk way ) kwenye ziwa Manyara
kutoka dola za Marekani 60 mpaka 10 kwa raia wa kigeni huku raia wa
nchi za Afrika Mashariki tozo hiyo imepungua kutoka shilingi 15, 000
mpaka shilingi 10,000.
Shelutete alisema serikali imetangaza tozo za hifadhi mpya
zilizoanzishwa mwaka 2019 za Burigi -Chato, Ibanda – Kyerwa na
Rumanyika – Karagwe , Mto Ugala, Nyerere na Kigosi.

Alisema kwa ujumla mabadiliko ya tozo hizo yamelenga  kuongeza
idadi ya wataliu, mapato pamojs na kuboresha huduma za utalii ndani
ya hifadhi.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Mawasiliano wa

Shirika la Hifadhi za Taifa nchini, (TANAPA),  Pascal
Shelutete leo akiongea na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya
shirika hilo jijini Arusha.