Tanzania kuendeleza ushirikiano na azaki afrika mashariki ili kukuza uchumi

Waziri Dkt Dorothy Gwajima akitoa hotuba yake kwenye la Jumuiya ya Azaki Afrika Mashariki, akiwa amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan

 Na Seif Mangwangi,Arusha

SERIKALI imesema itaendelea kukuza ushirikiano na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kwa kutunga sera ambazo zitakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Aidha Jumuiya ya Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ukanda wa Afrika Mashariki imetakiwa kusaidia nchi zao kubunj miradi ya maendeleo na kukuza uchumi.

Kauli hiyo ilitolewa  jana Jijini hapa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum,Dkt. Dorothy Gwajima, kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati akifungua kongamano la kwanza la Jumuiya ya Asasi za Kiraia ya Afrika Mashariki, unaoendelea jijini Arusha kwa siku tatu.

“Serikali ya Tanzania imeridhia kukuza ushirikiano na watendaji wasiokuwa wa kiserikali ili kutunga sera za kuzingatia wananchi pamoja na kukuza ukuaji wa uchumi wa jamii katika kanda ya Afrika Mashariki,”alisema Waziri huyo.

Waziri Gwajima,alisema kwa mujibu wa mkataba wa EAC unasema kuwapo kwa ushirikiano wa kikanda na maendeleo katika jumuiya ambao utazingatia watu na uendeshaji wa masoko ya kibiashara.

Hata hivyo, alisema serikali ya Tanzania inaamini kuwa kongamano hilo,litaandaa mikakati ya wazi ya ushirikishwaji ili kuhakikisha kuna kuwapo kwa ushiriki wa Azaki kama sauti ya wananchi katika ngazi ya kikanda.

“Tunaamini kwa dhati kwamba ushiriki wa watu kupitia Azaki ni muhimu katika kuhakikisha sera zinafanya kazi mashinani kwa kuwa tunatambua nafasi na umuhimu wa Asasi za Kiraia kufanya utafiti na mijadala ya mikutano ya hadhara kuhusu masuala muhimu yanayohusu wananchi,”aliongeza Waziri Gwajima.

Alisema eneo la Biashara Huria katika Bara la Afrika (AfCFTA), ni mpango maalum uliowekwa kurahisisha ushirikiano wa kiuchumi wa Afrika na biashara za ndani na kujenga uthabiti dhidi ya majanga ya kimataifa.

Washiriki wa kongamano la Azaki Afrika Mashariki wakifuatilia hotuba za ufunguzi

Dkt Gwajima alisema kuhusu wanawake na vijana  AfCFTA imedhamiria kuwa ya mabadiliko kwa kuwa itachangia ukuaji wa maendeleo endelevu barani Afrika.

Kwa upande wake Rais wa Asasi za Kiraia za Afrika Mashariki, Wakili  Daniel Lema, alisema lengo la kongamano hilo, ni kuzikutanisha pamoja Asasi hizo kwa kuwa sehemu ya kiungo baina ya wananchi wa eneo hilo na vyombo vinavyosukuma shughuli za mtengemano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Alisema Jumuiya hiyo ina malengo mahususi ya  kusaidia kupunguza na kuondoa kabisa pengo lililoko kati ya watu, Asasi za Kiraia, Serikali na vyombo vinavyofanya kazi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Pia katika kongamano hili,washiriki watapata fursa ya kukutana na wawakilishi kutoka kwenye nchi zao kujadiliana malengo ya kila nchi kwenye jumuiya kwa lengo la kujaribu kuleta uelewano baina ya asasi za kiraia, Serikali wanachama wa jumuiya juu ya malengo mahususi tutakayofanyia kazi,”alisema Lema.