Tanzania mbioni kuanza minada ya madini ya vito

 *MINADA MADINI YA VITO MBIONI KUANZA*

*#Kampuni ya Tanzanite Experience kinara Utangazaji Madini ya Vito*

*#Dkt. Biteko asisitiza wadau kuwekeza uongezaji thamani madini*

Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, Serikali iko mbioni kuanzisha upya Minada ya Madini ya Vito ili kuleta wanunuzi wakubwa, wafanyabiashara  na wachimbaji wa madini hapa nchini.

Hayo yamebainishwa Januari 5, 2023 wakati akizindua duka la utalii wa madini la kampuni ya Tanzanite Experience katika eneo la Manyara Kibaoni wilaya ya Karatu Mkoani Arusha 

Amesema kupitia mnada huo kampuni ya Tanzanite Experience kupitia duka la utalii wa madini itapata madini mengi kwa ajili ya kuendeleza kituo hicho na maeneo mengine anayoyafanyia kazi.

Dkt. Biteko amesema kuwa, kupitia kituo hicho kilichopo katika ukanda wenye maeneo ya hifadhi imekuwa ni sehemu kubwa ya kivutio cha utalii kwa wageni kutoka ndani na nje ya nchi. 

“Madini ya Tanzanite yamekuwa yakinunuliwa hapa nchini kwa kiasi kikubwa na watalii wanaokuja kutembelea hifadhi zetu na kupitia wao madini haya yanaendelea kutangazwa duniani,” amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa, Wizara ya Madini inapongeza uwekezaji huo ambao umefanywa kwa asilimia 100 na watanzania wakiunga juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan wakati akitangaza vivutio mbalimbali vilivyopo hapa nchini kupitia filamu ya “The Royal Tour” ambapo utalii na madini ya Tanzanite ilikuwa miongoni wa vivutio hivyo.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema wizara inahamasisha uwekezaji wa namna hiyo ambao unaunga mkono moja kwa moja jitihada zinazofanywa na Serikali za kutangaza madini ya Tanzanite duniani hususan katika eneo la shughuli za uongezaji thamani.

“Duka hili linatarajia kuuza bidhaa mbalimbali za madini ya Tanzanite na Tsavourite ambazo kwa miaka mingi zimekuwa zikitengenezwa na kuuzwa nje ya nchi. Hii ni hatua kubwa ambayo nchi yetu inaendelea kuchukua katika kuhakikisha madini haya yanazalishwa hapa nchini,” ameongeza Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko ametoa wito kwa watu wote ambao wana nia ya kuwekeza kwenye uchongaji, ukataji wa madini kuwekeza kwenye uongezaji thamani wa madini ili madini hayo yaweze kutupatia ajira na kodi kubwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tanzanite Experience Hassinne Sajani amesema kuwa, duka hilo limekuwa kivutio kikubwa kwa watanzania na watalii  kutoka nje ya nchi ambao wananunua bidhaa za madini zilizopo. Aidha ameongeza kuwa, kampuni imeajiri wafanyakazi 80 na zaidi ya asilimia 80 ni wakazi wa maeneo ya Manyara Kibaoni.

Ameahidi kuongeza juhudi kuendelea kutangaza madini ya Tanzania ambayo ni zawadi kwa Watanzania ili madini hayo yaweze kupanda thamani duniani.

Kwa upande wake, Meneja wa Tanzanite Experience, Junaid Khan amesema kuwa, zaidi ya wageni 6000 wamefika kutembelea Kampuni ya  Tanzanite Experience  

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Karatu Dadi Kolimba amesema biashara ya madini imefunguka katika wilaya ya Karatu na kuongeza mapato na kueleza kuwa ameipongeza kampuni hiyo kwa kutoa ajira zaidi ya 80 kwa watanzania katika nafasi mbalimbali.