Tanzania yaomba misaada kambi za wakimbizi, kuendelea kupokea wakimbizi

Naibu waziri wizara ya katiba na Sheria Geofrey Pinda akifunga mkutano wa Kimataifa wa chama cha Majaji wanaoshughulikia wakimbizi na wahamiaji Afrika

 Na Seif Mangwangi, Arusha

SERIKALI ya Tanzania imezitaka jumuiya za Kimataifa zinazoshughulikia wakimbizi na wahamiaji kuziwezesha nchi zinazopokea wakimbizi kwa kuwa nchi hizo zimekuwa zikitumia gharama kubwa za kuwahudumia.

Akizungumza wakati wa kufunga mkutano wa kimataifa wa majaji wanachama wanaoshughulikia wakimbizi na wahamiaji ukanda wa Afrika, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Godfrey Pinda amesema  kuwahifadhi wakimbizi kunahitaji nguvu ya ziada ikiwemo rasilimali fedha.

” Kuhifadhi wakimbizi ni gharama kubwa sana, mbali ya kutumia rasilimali za nchi lakini kuna wakimbizi wanafanya hadi mauaji hasa pale wanapotafuta hifadhi kwa nguvu, tunashukuru wafu wetu wamekuwa na moyo wa ukarimu, wanawapokea na hata kuwagawia maeneo yao kwaajili ya kulima, tunaomba na wenyewe waangalie,”amesema.

Amesema hata hivyo pamoja na gharama kubwa  Tanzania bado itaendelea kupokea wakimbizi na wahamiaji kama ambavyo imekuwa ikifanya ikiwa ni muendelezo wa kutekeleza haki za binaadam na kujenga mahusiano na nchi jirani.

kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Wakimbizi nchini, Sudi Mwakibasi amesema idara yake imekuwa ikihakikisha wakimbizi wanaoingia katika nchi mbalimbali Afrika wanapata huduma stahiki za kibinaadam kama mikataba ya Kimataifa inavyoeleza 

Pia ametoa wito kwa  wadau mbalimbali kufanya utafiti wa ongezeko la wakimbizi duniani na kuja na suluhisho la kukomesha tatizo hilo ambalo limekuwa likiendelea kukua kila siku na kusababishwa na sababu tofauti.

 ” Ninaomba kumalizia kwa kuhimiza kuendelea kushikamana katika kushughulikia viini vya changamoto zinazopelekea uzalishaji wakimbizi na uhamiaji mseto barani Afrika,” Amesema.

 

Kwa upande Mwakilishi wa shirika la umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi Duniani, George Kuchio amesema kikao hicho cha Majaji kimekuja wakati muafaka na kwamba wale majaji ambao walikuwa hawajui mambo kuhusu wakimbizi wameyajua kupitia mafunzo waliyopewa.

Zaidi ya majaji 200 wanachama wa chama cha Majaji Afrika wanaoshughulikia wakimbizi na wahamiaji Afrika walikutana Jijini Arusha kwa lengo la kujadili mambo yanayohusu wakimbizi na wahamiaji pamoja mafunzo ya siku mbili kuhusu wakimbizi.