Afisa Usafirishaji, Idara ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri Majini (TASAC) Selina Motiki akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha |
Egidia Vedasto
Arusha
WATEJA wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) wametakiwa kujisajili katika uwakala huo ili kuwawezesha kujua haki zao na taratibu zinazotakiwa kufuatwa katika masuala ya usafirishaji mizigo kwa njia ya meli.
Akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya Usalama wa Wafanya kazi Mahala pa Kazi (OSHA) yaliyofanyika Jijini Arusha Afisa Usafirishaji, Idara ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri Majini, Selina Motiki, amesema ni muhimu mteja kufahamu haki zake kwa lengo la kuondoa migogoro kati ya watoa huduma na wateja.
Amesema huduma zinazotolewa na wakala huyo wa Meli nchini (TASAC) ni pamoja na kudhibiti watoa huduma, kudhibiti mawakala wa meli, kudhibiti mawakala wa ugomboaji na uondoshaji mizigo baharini, kudhibiti wakusanyaji na watawanyaji mizigo.
Huduma zingine ni kudhibiti watoa huduma ndogondogo bandarini, kudhibiti wahakiki bandarini, sambamba na kudhibiti wanaotoa leseni, kuhuisha na kufuta leseni, kuweka viwango vya huduma na vigezo kwa watoa huduma.
“Sambamba na majukumu hayo niliyoyataja pia tunashughulikia malalamiko, ikitokea kuna mteja amepata changamoto basi tunawasiliana na mlalamikiwa na kuhakikisha kunapatikana ufumbuzi wa haraka, hii yote ni kumfanya mteja wetu ajivunie huduma tunazozitoa” amesema Motiki.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano Mwandamizi Shirika la Uwakala Tanzania (TASAC) Amina Miruko, ameeleza kuwa wanafanya kazi zao kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha usalama wa abiria, vyombo na mizigo kwa viwango vya kimataifa.
Ameongeza kwamba licha ya usimamizi huo, wanahakikisha kuwepo kwa vifaa vya uokoaji ili kuepuka ajali zisizo za lazima na kuwa na vyombo vya ukaguzi kwa lengo la kubaini uharifu.
“Ikumbukwe (SUMATRA) ilikuwa na majukumu ya kusimamia usafiri wa nchi kavu na majini, lakini baadae kulifanyika mgawanyo wa majukumu, (LATRA) kusimamia usafiri wa nchi kavu na (TASAC) kusimamia usafiri wa majini na ilianza kufanya kazi rasmi 23, Februari 2018” amesema Miruko.
Amefafanua kuwa, (TASAC) ina majukumu ya kuratibu utafutaji na uokoaji inapotokea dharura, TPA na wadau mbali mbali wa uokoaji huwa wanahusishwa ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Usafiri wa Maji Zanzibar (ZMA) ili kuokoa abiria na mali zao.
Ameongeza kwamba, wanashirikiana na wadau mbalimbali wa serikali na wasio wa serikali lengo kuwapa elimu wananchi kufahamu shughuli zinazofanywa na Uwakala wa Meli Tanzania.
Wakati huohuo Afisa Ugomboaji na Uondoshaji wa Shehena kutoka Shirika hilo Kisamo Mandari amesema pamoja na majukumu mengine, TASAC ina majukumu ya kibiashara chini ya biashara za meli ambazo ni ugomboaji na uondoshaji shehena za madini/maknikia, uondoshaji na ugomboaji nyara za serikali.
“Pamoja na hayo tunafanya uondoshaji na ugomboaji wa wanyama hai, vilipuzi na silaha, tukiwa na dhamira ya kuhakikisha kunakuwepo huduma za biashara na usafiri wa majini zilizo salama, za kuaminika, zenye uhakika na mazingira rafiki katika kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii” ameeleza Mandari.