Trafiki kutosimamisha magari ya utalii, rpc ataka apelekewe majina ya trafiki wasumbufu

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Constantine Kanyasu

Na Mwandishi Wetu, APC BLOG ARUSHA 
SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema itaendelea kupunguza adha mbalimbali  zinazowakabili Wadau wa Utalii likiwemo suala la  polisi wa usalama barabarani kusimamisha magari yenye watalii mara kwa mara.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu alipokuwa akizungumza na Wadau wa Utalii nchini  katika kongamano la Utalii lililofanyika mkoani Arusha.

Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa utalii nchini imejenga vituo vya ukaguzi wa magari vya utalii ili kupunguza usumbufu kwa watalii barabarani.

Amesema vituo  hivyo vitashughulikia masuala ya msingi likiwemo suala madereva wenye watalii kupimwa kilevi.

Amesema mbali na kilevi, Vituo hivyo vitashughulikia vitendo vyote ya uhalifu watakavyofanyiwa watalii.

Aidha, Mhe.Kanyasu amesema lengo la Serikali ni kupunguza kero kwa watalii ili wafikie milioni mbili mwaka 2019.

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Mhe.Kanyasu amesema licha ya  kujengwa vituo hivyo  vya ukaguzi lakini  bado kuna kero ambazo  zinafanyiwa  kazi lengo likiwa ni kuboresha sekta ya utalii.

Kwa upande wake, Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Jonathan Shana amewataka wadau wa utalii kufuata sheria lakini akataka kupewa taarifa za polisi wanaowakwaza.

“Nipigieni simu hata saa nane za usiku kwa askari wanawaomba rushwa nishughulike nao” Alisisitiza Shana.

Naye Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe.Mrisho Gambo amesema lengo la Arusha kuanzisha vituo vya ukaguzi magari ni kupunguza kero.

Amesema uwepo wa vituo hivyo vitafanya  mazingira bora kwa  watalii na wafanyabiashara.

Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji Watalii (TATO) Wilbard Chambulo amesema ujenzi wa vituo hivyo ni hatua muhimu ya kuwahakikishia watalii usalama wao pindi  wakiwa barabani pamoja na mali zao.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Prof.Adolf Mkenda amesema mkoa wa Arusha ni mfano wa kuigwa kwa mikoa mingine kwa kujenga vituo hivyo ili kupunguza kero kwa watalii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *