Unyanyapaa kwa wenye virusi vya ukimwi bado changamoto singida

Mganga Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk Victorina Ludovick akiwa kwenye moja ya mikutano ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya Ukimwi na umuhimu wa kila mtu kupima ili kujua hali ya afya yake

 

Na Abby Nkungu, Singida

Tatizo la unyanyapaa katika jamii, usiri mkubwa baina ya wajawazito na wenza wao pamoja na ushiriki mdogo wa wanaume kwenye huduma za afya ya uzazi na makuzi ya mtoto, kumetajwa kuwa miongoni mwa changamoto katika utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa kuzuia maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa UKIMWI kutoka mama kwenda kwa mtoto mkoani Singida.

Hayo yalibainishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Victorina Ludovick katika mahojiano maalumu na Mwandishi wa habari hizi juu ya uzuiaji wa maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Mpango huo.

Dk Ludovick alisema kuwa licha ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kupungua mwaka hadi mwaka mkoani Singida hadi kufikia asilimia 0.7 kwa takwimu za mwaka jana 2022, bado kuna changamoto katika utekelezaji wa Mpango huo wa Kitaifa.

“Kuna changamoto ya unyanyapaa wa ndani; yaani kwa mama mwenyewe, unyanyapaa kutoka kwa watu wa nje, usiri kati ya mjamzito na  mwenza wake iwapo mmojawapo anabainika kuwa na VVU na ushiriki hafifu wa wanaume kwenye huduma za afya ya uzazi na makuzi ya mtoto” alisema na kuongeza;

“Masuala hayo ni kikwazo katika utelekezaji wa Mpango wa Taifa wa kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto”

Hata hivyo, alieleza kuwa idara hiyo  inaendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa akinamama kuhudhuria kliniki na wenza wao pindi wanapokuwa wajawazito ili kupimwa na kupewa ushauri kulingana na hali zao na kuanzishiwa dawa na lishe kwa wanaobainika kuwa na VVU ili kulinda afya zao na mtoto.

“Wiki iliyopita mkoa wa Singida umezindua rasmi Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto inayoangazia maeneo matano ya mfumo wa malezi ya Afya bora, Lishe, Malezi yenye mwitikio, Fursa za ujifunzaji wa awali na Ulinzi na usalama kwa watoto kuanzia miaka 0 – 8; hivyo itasaidia kutia hamasa katika suala hili” alieleza.

Alisema kuwa kuwepo kwa wadau wengi katika Programu hiyo ili kutoa elimu na hamasa,  kuongezeka kwa vituo vya huduma za afya na upatikanaji mzuri wa dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI ni miongoni mwa mambo yanayoweza  kupunguza zaidi maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Baadhi ya wanufaika wanasema Mpango huo ni mzuri kwani unasaidia kuzaa watoto wasiokuwa na maambuzi ya virusi vya UKIMWI licha ya mzazi kuwa muathirika wa virusi hivyo na kwamba kikubwa ni kuendelea kutoa elimu zaidi kwa jamii ili kuondoa unyanyapaa unaojitokeza na kuleta athari mbalimbali.

“Mimi nilikuja hapa kliniki peke yangu baada ya kugundua tayari nina ujauzito, lakini nilipopimwa nikabainika kuwa na virusi vya UKIMWI, ninachomshukuru Mungu niliikubali hali yangu na kuanza dawa na kuzingatia ushauri wa wataalamu; ikiwemo kujifungulia kituo cha afya…. mtoto wangu huyo hapo mwaka wa tatu sasa, mzima kabisaa” alisema mama mmoja nje ya kituo cha afya kwa sharti la kutotajwa jina lake kwa kuogopa unyanyapaa.

Kupima afya kwa hiari ni jambo jema ili kujua hali yako kama afanyavyo mwananchi huyu katika picha hii
Wanandoa wakifurahia maisha kama kawaida hata baada ya kujua kuwa wana Virusi Vya Ukimwi (Picha: Kwa hisani ya Mtandao)

Mwanamke mwingine aliyejitambulisha kwa jina la mama Leila mkazi wa Kibaoni Singida mjini alisema baada ya kupimwa na kuonekana ana virusi vya UKIMWI, amekuwa akihudhuria kliniki kila mwezi  hadi kufikia miezi saba ya mimba yake hivi sasa na matarajio yake ni kupata mtoto asiyekuwa na maambukizi kwani tayari anatumia dawa na kuzingatia ushauri wote wa  wataalamu.

“Mimi tayari natumia dawa, nina furaha kubwa na matarajio yangu ni kupata mtoto asiyekuwa na maambuzi kwani tunazingatia yote tunayoelekezwa na manesi na madaktari. Huwa tunakuja kila mwezi kliniki na mume wangu kwa kuwa naye ana tatizo kama langu” alisema mama Leila na kushauri watu kutojificha majumbani pindi wanapopima na kujua hali zao kuwa wana maambukizi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la ESTL  linalotekeleza Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto mkoani Singida, Joshua Ntandu anasema wanaangalia namna ya kushirikiana na idara ya afya kujikita zaidi katika  kutoa elimu.

Alifafanua kuwa lengo ni kuhakikisha wajawazito  wenye virusi vya UKIMWI wanafuata ushauri wa wataalamu, matumizi sahihi ya dawa za kufubaza virusi za ARV, lishe bora, kuhudhuria kliniki na wenzi wao na kujifungulia kwenye huduma za afya ili kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Mpango wa Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa ajili ya kupunguza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto unaotekelezwa nchi nzima, ulianzishwa mwaka 2003 kabla ya kufanyika mapitio mwaka 2019 kuuboresha ili uweze kuainisha zaidi walengwa wake.