|
Mkurugenzi mtendaji wa UTPC Kenneth Simbaya akiongoza zoezi la uzinduzi wa kampeni ya kupinga Ukatili wa kijinsia.
|
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (Union of Tanzania Press Clubs – UTPC) umezindua Kampeni Maalumu ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Lengo la kampeni hiyo ni kupaza sauti za wasichana, wanawake na watoto dhidi ya vitendo vya ukatili katika mikoa yote ya Tanzania kutokana na kwamba Vyombo vya habari vina nguvu ya kusaidia ustawi wa jamii.
Uzinduzi huo umefanyika leo Novemba 25,2023 mkoani Morogoro wakati wa semina ya waandishi habari juu ya ukatili wa kijinsia iliyoratibiwa na UTPC kwa kushirikisha wanahabari 28 kutoka Tanzania bara na visiwani.
Mwenyekiti wa Mipango na fedha UTPC na Katibu Mtendaji wa Klabu ya waandishi wa Habari Mkoa wa Morogoro, Lilian Lucas amesema waandishi wa habari hawapaswi kukata tamaa katika kupaza sauti dhidi ya matukio na vitendo vya ukatili kwa wasichana ,wanawake ,watoto na hata wanaume wanaofanyiwa ukatili sasa kuwa ni wajibu wakutetea haki kwa makundi yote.
“Tusikate tamaa katika kuendelea kuwasemea wanawake,wasichana na watoto kwa kuwa yapo matukio mengi ya kupigwa ,kubakwa , kulawitiwa na vitendo vingine vya kikatili. Sisi waandishi wa habari ni nafasi yetu ni kuendelea kuisemea jamii kwa kupaza sauti kwa kazi tunazofanya”, amesema Lilian.
Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC,Kenneth Simbeye amesema vyombo vya habari vinatoa nafasi kwa jamii kuendelea kufikiri zaidi kwa kile kinachoripotiwa kila wakati dhidi ya vitendo vya matukio ya ukatili wa kijinsia.
“Vyombo vya habari vinawapa watu namna ya kufikiri dhidi ya matukio ya vitendo vya ukatili na katika makundi mbalimbali ndani ya jamii na tuwe na faraja kuendesha kampeni hii kwa ajili ya kupaza sauti ili kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake,wasichana na watoto” ,amesema Kenneth.
“Wanahabari tunalo jukumu la kuwa mstari wa mbele kuwasemea wanawake,wasichana na watoto kwa kupaza sauti katika mikoa yetu ili wasiendele kuathirika na vitendo vya kikatili”, amesema Kenneth.
Nao Waandishi wa habari wameshauri uongozi wa UTPC kuweka mpango wa ufuatiliaji wa habari za ukatili zinazoripotiwa kupitia klabu za waandishi wa habari na kisha kuweka mpango wa muda mrefu wa kupaza sauti.
“Tuweke mpango mzuri wa muda mrefu wa kupaza sauti kwa vyombo vya habari utakaoweza kuratibiwa na UTPC kupitia klabu za waandishi wa habari zinazosimamiwa na UTPC”, amesema Zulfa Mfinanga.