Na, Asha Shabani.
Licha ya kuwepo kwa habari za mtandaoni zinazodai kuwa Mbunge wa kuteuliwa na Rais, Humphrey Polepole kujiuzulu nafasi yake, Mbunge huyo amekanusha madai hayo huku akisema mwaka 2025 hatogombea ubunge katika jimbo lolote Tanzania.
Habari hizo za uzushi ambazo zimekuwa zikienezwa katika mtandao wa YouTube zilianza kusambazwa mwanzoni mwa Oktoba baada ya Polepole akiwa katika mkutano wa vijana mkoani Arusha kuwa hatogombea kiti cha ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Ni kweli Polepole kajiuzulu?
Hakuna sehemu yoyote ambayo mbunge huyo ametangaza kujiuzulu zaidi ya kusema hatogombea ubunge 2025.
Wapotoshaji wametumia mkutano wa Arusha aliofanya Polepole na kumlisha maneno kuwa kajiuzulu, jambo ambalo siyo sahihi. Katika video ambayo alitoa kauli ya kutokugombea, hakuna sehemu yoyote ambayo ametangaza kujiuzulu nafasi yake.
https://www.youtube.com/watch?v=PXli8E80iu4 (
Pia tumetumia zana mbalimbali za kidijitali kuangazia madai hayo ikiwemo InViD, Google Image kubaini kama habari hiyo imeripotiwa na vyombo vingine vya habari au kama Polepole alitoa tamko hilo katika matukio mengine, huko nako hakuna taarifa kama hiyo.
Hivyo taarifa hiyo ya kujiuzulu kwa Polepole haina ukweli wowote. Huenda wapotoshaji walikuwa na malengo yao binafsi ikiwemo kujipatia watazamaji wengi, jambo ambalo ni kinyume na misingi ya uandishi wa habari.
Habari za upotishaji zisipodhibitiwa zinaweza kuleta madhara makubwa kwenye jamii hasa kwa afya za watu na ukuaji wa uchumi, hivyo waandishi wa habari hawapaswi kuwa sehemu ya kusambaza habari hizo bali kuzingatia maadili na taaluma zao.