HALMASHAURI ya wilaya ya Mufindi mkoani Iringa kwa kushirikiana na mradi wa Youth Angecy Mufindi (YAM) yatumia kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 14 kuwapatia msaada wa nguruwe vijana 80 wanaotoka katika mazingira magumu kwenye kata tatu za Luhunga, Ihanu na Mdabulo.
Akikabidhi jana msaada huo wa nguruwe meneja mradi wa YAM Zilipa Mgeni alisema kuwa mradi huo wa YAM umekuwa ukitekelezwa kwenye vijiji 16 vya kata tatu za Ihanu ,Luhunga na Mdabulo huku walengwa wakubwa wa mradi huo wakiwa ni vijana wanaotoka katika mazingira magumu ambao baadhi yao ni wale ambao wamekatisha masomo kutokana na changamoto mbali mbali za kimaisha.
Mgeni alisema vijana hao kabla ya kukabidhiwa mtaji wa nguruwe kwa ajili ya kwenda kufunga kama sehemu ya mradi wa kiuchumi kwao ,mradi huo uliweza kuwapatia elimu ya ujasiliamali pamoja na elimu ya afya ya akili ili kuweza kujitambua na kwenda kuondokana na maisha ya kushinda vijiweni bila kazi za kufanya kutokana na kukata tamaa ya maisha .
Alisema kuwa kupitia mradi huo wa miaka minne ulioanza mwaka jana vijana hao wataendelea kunufaika na mradi huo unaotekelezwa kwa ushirikiano mkubwa na serikali ya Halmashauri ya wilaya ya Mufindi.
Hivyo alisema Halmashauri ya Mufindi chini ya mradi wa Foxes Community and Wildlife Conservation( FCWC) na YAM kupitia ufadhili wa Finland utakelekelezwa kwenye kata za Luhunga ,Ihanu na Mdabulo ni mradi utakaonufaisha vijana na watoto wanaotoka katika familia duni zaidi ya vijana 770 atika vijiji 16.
Mgeni alisema kuwa vijana hao ambao wamepatiwa mtaji wa Nguruwe hao ni sehemu ya vijana 770 ambao watanufaika na mradi huo kwa kipindi chote cha miaka minne ya utekelezaji wa mradi huo katika kata hizo tatu za wilaya ya Mufindi.
Alisema kila kijana ambae ni mnufaika na mradi huo amepatiwa mtaji wa nguruwe mbili moja jike na nyingine dume pamoja na chakula cha kuhudumia nguruwe hao kwa kipindi cha mwezi mmoja wa mwanzo .
Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wenzake wa mradi huo Iren Chumi alisema kuwa msaada huo ni ukombozi mkubwa kwake kwani kwa muda alikuwa akitamani kuwa mfugaji wa nguruwe lakini changamoto kubwa hakuwa na elimu na mtaji wa kuendeshea shughuli hiyo ya ufugaji hivyo kupitia msaada huo wa YAM ni mwanzo kwake kupiga hatua ya kiuchumi pamoja na kutimiza ndoto yake.
Kaimu mtendaji wa kata ya Luhunga Vumilia Nyunza alipongeza mradi huo wa YAM na Halmashauri ya Mufindi kwa kuwafikia vijana hao wenye mazingira magumu na kuwa kupitia msaada huo ana amini vijana wengi waliokuwa wakishinda vijiweni sasa watajikita katika shughuli za uzalishaji mali.