Vijana wanaotoka kwenye mazingira magumu kata tatu za wilaya ya Mufindi wakiwa kwenye mafunzo ya ujasiliamali
ZAIDI ya vijana 80 wanaotoka katika mazingira magumu kata tatu za Igoda , Luhunga na Mdabulo wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wameanza kupatiwa mafunzo maalumu ya uanzishaji miradi ya kiuchumi itakayowawezesha kuendesha maisha yao na kusaidia familia zao.
Mafunzo hayo ya siku 10 yameanza jana katika ukumbi wa Yatima kijiji cha Igoda wilaya ya Mufindi kwa kushirikiasha vijana hao ambao baadhi yao ni wale ambao wamekatisha masomo kwa changamoto mbali mbali kimaisha ikiwa ni pamoja na mabinti waliokatisha kwa ujauzito .
Mkufunzi wa mafunzo hayo John Kalolo kutoka shirika lisilo la kiserikali la RLABS -Tanzania alisema kuwa mafunzo hayo maalum ni ya kuwajengea uwezo wa katika nyanja ya ujasiliamali yatawezesha vijana hao kuweza kuondokana na fikra mgando ambazo baadhi yao wamekuwa nazo kuwa ili uwe mjasiliamali ni lazima kuwa na fedha mkononi wakati unaweza kuwa mjasiliamali bila ya kuanza na mtaji wa fedha .
“Maeneo mengi ya vijijini kuna fursa nyingi za kufanya ambazo kimsingi ni moja kati ya mtaji mkubwa kwa mtu ambae anatamani kuwa mjasiliamali hivyo iwapo wahusika wataondokana na fikra mgando za kutegemea fedha wanaweza kupiga hatua katika maisha” alisema
Kuwa ili vijana hao waweze kuondokana dhana hiyo potofu ni lazima kwanza kujitambua na kujiamini kabla ya kuanza shughuli ya ujasilimali ambayo anahitaji kuifanya na baada ya kuanza ndipo wanaweza kuanza mchakato wa pili wa kuomba mikopo ya kuboresha shughuli husika ya ujasiliamali.
Hata hivyo alisema kupitia ardhi walizonazo vijijini ziwe za familia ama zao binafsi wanaweza kubuni miradi ya kiuchumi ambayo miradi hiyo haihitaji mtaji mkubwa wa fedha zaidi ya kuhitaji nguvu kazi ya mkono.
Kalolo alisema mfano ujasiliamali wa ususi kwa mabinti ni ujasiliamali ambao mtu anaweza kuanza kwa ubunifu usio tegemea fedha na baada ya kuanza ndipo wanaweza kuboresha kwa kutafuta eneo litakalohitaji fedha za kuboresha zaidi.
Akizungumzi faida ya mafunzo haya meneja wa mradi wa Youth Agency Mufindi (YAM) Zilipa alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha vijana zaidi ya 770 wakiwemo watoto 150 yatima kutoka kata hizo tatu ambazo zote zitaunganishwa na vijiji 16 za mradi huo .
Alisema mradi huo wa YAM ni wa miaka minne toka mwaka 2021/2024 umefadhiliwa na serikali ya Filands chini ya taasisi yake ya Diaconess kwa ushirikiano wa serikali ya Tanzania chini ya Halmashauri ya wilaya ya Mufindi na taasisi ya Foxes Community and Wild Life Conservation.
Mgeni alisema baada ya mafunzo hayo kutolewa kwa walengwa watawezeshwa mitaji ya kuendeshea miradi ambayo watakuwa wamechangua kuifanya kwa kuwaongezea nguvu ya kuiboresha zaidi.
Wilaya ya Mufindi ni moja kati ya wilaya tatu za mikoa wa Iringa ambazo zimekuwa na changamoto ya vijana na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kupitia serikali na wadau mbali mbali wa maendelea wameendelea kuwawezesha vijana hao ili kuanzisha miradi ya kiuchumi inayowafanya kupiga hatua za kimaendeleo .