Vijana wanufaika na mfuko kuendeleza ujuzi sdf

 VIJANA WANUFAIKA NA MFUKO KUENDELEZA UJUZI SDF

Na Jane Edward, Arusha 

Vijana nchini wameendelea kunufaika na Mfuko wa kuendeleza ujuzi(SDF) unaoratibiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) unaolenga kuwezesha Taasisi zinazotoa  mafunzo ya kuongeza ubora na ufanisi katika kutoa mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi katika sekta sita za kipaumbele nchini.

Aidha Mfuko wa SDF ambayo ni sehemu ya Programu ya kuendeleza Elimu ya Ujuzi na Mafunzo ya Stadi za kazi zenye kuleta tija katika ajira na mpango mkakati wa kitaifa wa kukuza na kuendeleza ujuzi nchini bado una malengo ya kuongeza vijana zaidi kujiunga na mpango huo.

Afisa habari wa TEA,Eliafile Solla ameyasema hayo katika Maonesho ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi yanayofanyika kwenye viwanja  vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Solla amesema kuwa, mfuko huo unawawezesha vijana kuendeleza ujuzi wao na uwezo wa kujishughulisha na shughuli za kiuchumi ili waweze kujiajiri na kuajiri wengine .

Amesema kuwa,Mfuko huo unatoa ufadhili kwa Taasisi zinazolenga kutoa mafunzo ya kuendeleza ujuzi katika sekta sita za kipaumbele zinazoratibiwa na Programu ya ESPJ ambazo ni kilimo na kilimo uchumi,utalii na huduma za ukarimu,uchukuzi,ujenzi ,Teknolojia ya habari na Mawasiliano (TEHAMA)pamoja na Nishati .

Solla ameongeza kuwa,mradi wa SDF hutekelezwa ndani ya mwaka mmoja ambapo Taasisi nufaika inatakiwa kuendesha mafunzo mafupi ya mwezi mmoja hadi miezi mitatu kwa makundi tofauti hadi kufikia idadi ya wanufaika iliyowekwa kwa Taasisi husika.

Amesema kuwa, kupitia mfuko huo vijana wengi wamefanikiwa  kwa kiasi kikubwa kwani wameweza  kujiajiri na wengine kutengeneza ajira kwa wengine na hivyo kuondokana na changamoto ya ajira iliyopo nchini.